• HABARI MPYA

    Monday, October 05, 2015

    KILA MCHEZAJI AZAM FC ANA UMUHIMU WAKE, ASEMA STEWART HALL

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amesema kwamba wachezaji wote waliomo katika kikosi chake, wamo katika mipango yake na kila mmoja atapata nafasi ya kucheza wakati wake ukifika.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo, Hall amesema kwamba kikosi chake cha kwanza kina wachezaji 28 na bado vijana wa timu ya pili, wasiopungua watano wamepandishwa, hivyo hawezi kuwatumia wote kwa wakati mmoja.
    “Watu wanashangaa kuona baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa wanakaa benchi, wanaona kama hawana thamani. Hapana, kila mchezaji aliyesajiliwa Azam FC ana thamani na anahitajika,”amesema Hall.
    Stewart Hall (kushoto) na benchi zima la Ufundi Azam FC

    Hall amesema kwamba anahitaji kutumia wachezaji wasiozidi 14 katika mchezo mmoja na katika kikosi cha sasa cha Azam FC, wachezaji wote ni wakubwa.
    “Farid (Malik) alikuwa mchezaji asiye na umaarufu Azam FC wakati tunaanza msimu huu. Lakini sasa naye ni mchezaji mwenye jina kubwa. Kevin (Friday), Bryson (Raphael), Mudathir (Yahya) ni miongoni mwa wachezaji wadogo Azam FC, lakini tayari wana majina makubwa,”amesema.
    Hall amesema kwamba hakuna mchezaji mdogo Azam FC na wote wana uwezo, na kwamba hilo ndilo jambo ambalo anajivunia kwa sasa katika timu yake.
    “Unapokuwa na kikosi cha aina hii, unajiona kabisa wewe ni mshindani wa mataji. Nazungumza na wachezaji wangu na wanajua hali halisi, nachotazama ni nini nahitaji katika wakati gani kutoka kwao,”amesema.
    Akiizungumzia Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoendelea huku Azam FC na mabingwa watetezi, Yanga SC zikiwa timu pekee ambazo hazijapoteza pointi hadi sasa, Hall amesema; “Bado mapema”.
    “Baada ya mechi yetu na Yanga sasa tunaweza kuanza kusema chochote, lakini kwa vyovyote ligi ni ngumu. Kila timu inataka kuifunga Azam FC, kila mechi kwetu ni ngumu,”amesema.
    Hall amesema dhamira ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwishoni mwa msimu na atapambana na changamoto zozote kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri.
    Azam FC iliyomaliza nafasi ya pili msimu uliopita, itamenyana na Yanga SC na Oktoba 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo ambao utazitenganisha timu hizo kwenye nafasi kileleni. 
    Azam FC ina pointi 15 sawa na Yanga SC inayoongoza kwa wastani wa mabao, baada ya timu zote kushinda mechi zao zote tano za awali.
    Kikosi cha Azam FC kilichoifunga Mbeya City 2-1 katika mchezo wake uliopita

    KIKOSI CHA AZAM FC 2015;
    Makipa; Mwadini Ali, Aishi Manula na Mtacha Mnata.
    Mabeki; Aggrey Morris, Said Mourad, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Serge Wawa, 
    David Mwantika, Shomari Kapombe, Bryson Raphael na Abdallah Kheri.
    Viungo; Frank Domayo, Mudathir Yahya, Khamis Mcha, Himid Mao, Farid Malik, Salum Abubakar, Jean Mugiraneza, Ramadhani Singano, Kelvin Friday na Kipre Bolou. 
    Washambuliaji; John Bocco, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche, Ame Ali na Allan Wanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA MCHEZAJI AZAM FC ANA UMUHIMU WAKE, ASEMA STEWART HALL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top