• HABARI MPYA

  Sunday, March 10, 2019

  YANGA SC YAENDELEA KUJIKUSANYIA POINTI LIGI KUU, YAICHAPA KMC 2-1

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa 2-1 KMC jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Yanga inayofundishwa na kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ifikishe pointi 67 baada ya kucheza mechi 27, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 11 zaidi ya Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili.
  Mabingwa watetezi, Simba SC wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa tena taji msimu huu, kwa sasa wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 51 za mechi 20, mbele ya KMC inayobaki na pointi zake 41 za mechi 29. 
  Haukuwa ushindi mwepesi kwa Yanga leo, kwani ililazimika kutoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa bao la dakika ya 16 la mshambuliaji anayecheza kwa mkopo KMC kutoka Simba SC, Mohammed Rashid.
  Rashid aliuwahi mpira alioukosa kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko baada ya kuuetelezea kujaribu kuokoa na kumpiga chenga mchezaji mwingine wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kabla ya kumchambua kipa Mkongo, Klaus Kindoki.
  Yanga SC ilisawazisha bao hilo dakika ya 37 kupitia kwa kiungo wake Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi aliyeunganishwa kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto Gardiel Michael aliyeanzishiwa kona fupi na kiungo Deus Kaseke.
  Kipindi cha pili kipa Mrundi wa KMC, Jonathan Nahimana alishindwa kurudi uwanjani baada ya kumaliza kipindi cha kwanza akiugulia maumivu na nafasi yake kuchukuliwa na kipa namba moja wa zamani wa Tanzania, Juma Kaseja.
  Beki Ally Ally akaifungia Yanga bao la ushindi dakika ya 66 baada ya kujifunga kwa kichwa cha mkizi akijaribu kuokoa krosi ya Ibrahim Ajibu aliyomuingizia mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.
  KMC walipambana kujaribu kusawazisha bao hilo huku Yanga wakisaka mabao zaidi, lakini pande zote mbili ziliishia kwa kukosa mabao ya wazi.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Said Juma ‘Makapu’ dk81, Papy Kabamba Tshishimbi, Herirtier Makambo, Thabani Kamusoko/Amissi Tambwe dk63 na Deus Kaseke/Ibrahim Ajibu dk63. 
  KMC; Jonathan Nahimana/Juma Kaseja dk46, Aaron Lulambo, Ally Ramadhani, Ally Ally, Karos Kirenge, Ally Msengi, George Sangija/Abdul Hillary dk81, Mohammed Rashid, Emmanuel Mvuyekure, Charles Ilanfya/James Msuva dk59 na Hassan Kabunda. 
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Mwadui FC imeutumia vyema Uwanja wa nyumbani wa Mwadui Complex wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Mbeya City.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAENDELEA KUJIKUSANYIA POINTI LIGI KUU, YAICHAPA KMC 2-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top