• HABARI MPYA

    Tuesday, April 03, 2018

    BOCCO AING’ARISHA SIMBA SC, AFUNGA MABAO YOTE NJOMBE YAFA 2-0 SABA SABA

    Na Princess Asia, NJOMBE
    SIMBA SC imejitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Njombe Mji FC jioni ya leo Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.
    Pongezi kwa mfungaji wa mabao hayo yote mawili leo, Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’, moja kila kipindi na sasa Wekundi wa Msimbazi wanafikisha pointi 49 baada ya kucheza mechi 21, wakiwazidi kwa pointi tatu mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46 za mechi 21 pia.  
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa chipukizi Meschak Suda kutoka Songea, aliyesaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bocco alifunga bao la kwanza kwa shuti la mguu wa kulia kufuatia kuudondosha chini kwa kichwa mpira mrefu wa adhabu uliopigwa na beki Yussuf Mlipili.
    Bao hilo lilionekana kuwavuruga Njombe Mji FC na kujikuta wanawaruhusu Simba kutawala mchezo zaidi na kukaribia kufunga mara kadhaa.
    Lakini dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika SImba wakiwa mbele kwa hilo moja tu na kipindi cha pili hakukuwa na mabadiliko yoyote kwa Njiombe Mji FC kimchezo, kwani Wekundu wa Msimbazi waliendelea kutawala mchezo.
    Haikuwa ajabu Bocco tena alipowainua mashabiki wa Simba kushangilia bao la pili baada ya kufunga vizuri dakika ya 64 kwa guu la kulia kufuatia pasi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe.
    Kocha Mfaransa, Pierre Lechantre akawaingiza wachezaji wawili, majeruhi wa muda mrefu, beki Salim Mbonde na kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima kumalizia mchezo. 
    Kikosi cha Njombe FC kilikuwa; David Kissu, Christopher Kasewa, Steven Mwaijala/Agathon Mapunda dk80, Hussein Akilimali, Peter Mwangosi, Jimmy Mwasondola, Awadh Salum, Mustapha Bakari, Ettienne Ngladjoe/Rafael siame dk70, David Obashi na Ditram Nchimbi.
    Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Juuko Murshid, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei/Salim Mbonde dk60, Shomary Kapombe, Emmanuel Okwi/Laudit Mavugo dk52, John Bocco na Shiza Kichuya/Haruna Niyonzima dk81.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO AING’ARISHA SIMBA SC, AFUNGA MABAO YOTE NJOMBE YAFA 2-0 SABA SABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top