• HABARI MPYA

    Friday, January 19, 2018

    SIMBA TAYARI WAKO BUKOBA KUIVAA KAGERA JUMATATU, KOCHA MPYA ASAINI MKATABA NA KUAHIDI RAHA MSIMBAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Simba SC kimewasili mjini Bukoba kwa ndege leo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Jumatatu.
    Simba imeingia Bukoba siku moja tu baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Singida United katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji wake mahiri, Mganda Emmanuel Okwi akifunga mabao mawili.
    Ushindi wa jana unaifanya Simba SC ifikishe pointi 29, baada ya kucheza mechi 13, ikiwazidi pointi saba mabingwa watetezi, Yanga SC na pointi mbili Azam FC wenye 27 katika nafasi ya pili, wakati Mtibwa Sugar sasa ni ya tatu kwa pointi zae 24 baada ya timu zote kucheza mechi 13.
    Na sasa Wekundu wa Msimbazi kwa kuhakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi, wamewasili mapema Bukoba kwa usafiri wa haraka ili kufanya maandalizi mazuri.
    Wachezaji wa Simba SC wakiwasili Uwanja wa ndege wa Bukoba leo

    Wakati kikosi kikiwasili mjini Bukoba, Jijini Dar es Salaam Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amemtambulisha kocha mpya Mfaransa, Pierre Lechantre pamoja na Msaidizi wake,  kocha wa mazoezi ya viungo, Mmorocco Mohammed Aymen Hbibi. 

    Katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa Kivukoni, hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam, Abdallah alimsainisha mkataba Lechantre, ambao hata hivyo hawakusema wa muda gani.
    Abdallah amesema kwamba Mfaransa huyo anaingia Simba SC kwa ajili ya programu maalumu ya kuinoa timu ya wakubwa na wadogo.
    Lechantre ambaye ataanza kazi timu itakaporejea kutoka Bukoba, amesema anaomba apewe angalau miezi minne ili wana Simba waanze kufurahia kazi yake. 
    Mabeki, Mganda Juuko Murshid na mzawa 

    Mohammed Hussein 'Tshabalala' wakiwa 
    kwenye ndege leo
    Pierre Lechantre aliyezaliwa Aprili 2, mwaka 1950 mjini Lille, Nord, Ufaransa ni kocha aliyeipa Cameroon ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2000 na kabla ya kuanza kufundisha alikuwa mchezani pia.
    Aprili 27 mwaka 2012, Lechantre alitambulishwa kuwa kocha Mkuu wa Senegal, lakini akashindwa kufikia makubaliano ya mwisho na Shirikisho la Soka la nchi hiyo.
    Akiwa mchezaji katika nafasi ya ushambuliaji, Lechantre amechezea klabu za Paris FC (1986–1989), Red Star 93 (1983–1986), Stade de Reims (1981–1983), Olympique de Marseille (1980–81), RC Lens (1979–80), Stade Lavallois (1976–1979), AS Monaco (1975–76), FC Sochaux (1970–1975) na Lille OSC (1964–1970).
    Na akiwa kocha amefundisha timu za taifa za Kongo (2016), Cameroon (1999-2001), klabu za Al-Ittihad Tripoli ya Libya kuanzia 2014 hadi 2015, Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi hadi September 2013, CS Sfaxien ya Tunisia kuanzia Juni hadi Desemba 2010, Club Africain ya Tunisia kuanzia Juni 10 mwaka 2009 hadi Aprili 2010 na Al Rayyan ya Qatar.
    Amefundisha pia timu ya taifa ya Mali kuanzia Machi hadi Oktoba 2005, Al-Siliya Sports Club ya Qatar kuanzia Novemba 2003, Al-Ahli ya Jeddah kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka 2003, Qatar kuanzia Juni 2002, Le Perreux (1992–1995) na Paris FC (1987–1992).
    Amewahi pia kuwa Mshauri wa Ufundi wa Val de Marne kuanzia Julai 7 mwaka 1995 hadi Januari 1999.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA TAYARI WAKO BUKOBA KUIVAA KAGERA JUMATATU, KOCHA MPYA ASAINI MKATABA NA KUAHIDI RAHA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top