• HABARI MPYA

  Monday, January 01, 2018

  AZAM FC YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI, YAICHAPA MWENGE 2-0

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imeanza vema harakati za kutetea ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuinyuka Mwenge mabao 2-0, mchezo uliofanyika usiku wa Jumapili Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Kwa ushindi huo, Azam FC imekaa kileleni mwa Kundi A ikiwa na pointi tatu sawa na Mwenge, ambayo ilipata ushindi kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Jamhuri, zote zikiwa ni timu kutoka Pemba.
  Benchi la ufundi la Azam FC liliutumia mchezo huo wa kwanza kuwapa nafasi wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza kwenye mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Stand United pamoja na wale waliocheza dakika chache.
  Mshambuliaji chipukizi wa timu hiyo, Paul Peter, ndiye aliyeibuka shujaa baada ya kufunga mabao yote mawili la kwanza akitupia dakika ya 41 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na mshambuliaji Bernard Arthur, aliyepiga shuti lililopanguliwa na kipa kabla ya mfungaji kuuwahi mpira na kumalizia.
  Peter aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, alifunga bao la pili dakika ya 62 akimalizia pia kwa shuti baada ya kukutana na mpira uliotemwa na kipa kufuatia shuti lililopigwa na Idd Kipagwile.
  Baada ya mchezo huo, Azam FC itashuka tena dimbani Jumatano ijayo kuvaana na Jamhuri ya Pemba, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan saa 10.30 jioni.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Saleh Abdallah, Hamim Karim, David Mwantika/Oscar Masai dk46, Yakubu Mohammed, Brison Raphael, Masoud Abdallah/Shaaban Idd dk84, Frank Domayo/Enock Atta Agyei dk76, Bernard Arthur, Paul Peter/Waziri Junior dk68 na Idd Kipagwile.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI, YAICHAPA MWENGE 2-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top