• HABARI MPYA

    Friday, December 01, 2017

    SIMBA WAMUALIKA MWAKYEMBE MKUTANO WA MABADILIKO JUMAPILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ESSALAAM
    KLABU ya Simba imemualika Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe katika mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika Jumapili kuanzia Saa 4:00 asubuhi kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Hajji Manara ameseam kwamba wanataka kuutumia mkutano huo kumtangaza mshindi wa zabuni ya uwekezaji katika klabu yao.
    Miezi miwili iliyopita klabu hiyo ilitangaza zabuni kwa wanachama wenye uwezo na mtaji kuanzia Sh. Bilioni 20 kujitokeza na kufanya uwekezaji katika klabu hiyo katika mchakato wa mabadiliko ya muundo wa uendeshaji hadi kuwa wa hisa.
    Waziri Dk. Harrison Mwakyembe amealikwa katika mkutano mkuu wa wanachama wa Simba kesho ukumbi wa Mwalimu Nyerere

    Alisema anaamini huo utakuwa ni mkutano wa kihistoria kwasababu wanakwenda kubadilisha muundo.
    “Tunapokwenda kubadilisha mfumo wa uendeshaji tunategemea klabu yetu itakuwa ni tajiri na kuwekeza kwenye miundombinu, itakuwa ina uwezo wa kununua wachezaji bora watakaowezesha kuwa na ligi bora Tanzania na kushinda mataji mengi klabu bingwa Afrika,”alisema.
    Awali, klabu hiyo ilisema mwekezaji atamiliki asilimia 50 ya hisa huku asilimia 10 zikitarajia kugawiwa kwa wanachama hai na nyingine 40 kuuzwa kwa wanachama.
    Tayari mfanyabiashara na mfadhili wa Simba Mohamed Dewji aliwahi kuonyesha nia ya kuwekeza iwapo tu atapewa asilimia 50 ya hisa, ingawa hata hivyo, kesho itajulikana kama atakuwa yeye au wengine kutokana na vigezo vilivyokuwa vimewekwa.
    Hata hivyo, kazi bado ipo kwa Simba kwani serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limefanya marekebisho ya kanuni zake na juzi kutoa waraka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unaotoa maelekezo ya ununuaji na uuzwaji wa hisa za klabu au Chama cha Michezo.
    Marekebisho yaliyopo ni kwamba Vyama au klabu zilizoanzishwa na wanachama vikiamua kuuza hisa zake vinapaswa kutenga asilimia 51 kwa ajili ya wanachama na asilimia 49 kwa wanaotaka kununua.
    Pia, wanatakiwa kupitia kwenye mamlaka ya mitaji na masoko ili kuidhinishwa na baadaye kurudi kwenye soko la hisa  ili kufuata taratibu za uuzwaji na ununuaji.
    Manara alisema tayari wamepata taarifa hiyo kutoka TFF na wanaendelea na mazungumzo na Dk. Mwakyembe kuhusu taratibu hizo mpya na namna ya kubadili kanuni wakati wakiendelea na mchakato wao wa kutangaza mwekezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAMUALIKA MWAKYEMBE MKUTANO WA MABADILIKO JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top