• HABARI MPYA

    Friday, December 01, 2017

    MSHAMBULIAJI WA ETOILE DU SAHEL AJIUNGA NA YANGA SC MIAKA MIWILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Yohana Oscar Nkomola amejiunga na mabingwa wa Bara, Yanga SC kwa mkataba wa miaka miwili.
    Nkomola anayesimamiwa na akademi ya Cambianso ya Dar es Salaam amesaini mkataba huo mapema wiki hii kabla ya kwenda Kenya na kikosi cha Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la CECAFA Challenge. 
    Kwa kusaini Yanga, Nkomola anakuwa mchezaji wa tatu kutoka kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki Fainali za Vijana za U-17 Afrika nchini Gabon mwezi Mei mwaka huu. 
    Yohanna Nkomola (kushoto) akiwa na mchezaji mwenzake wa timu ya vijana ya Etoile du Sahel ya Tunisia Septemba mwaka huu mjini Sousse  
    Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (kushoto) akiwa na Yohanna Nkomola (kulia)

    Wengine ni kipa Ramadhani Kabwili na kiungo Mussa Said ambao wote wanasajiliwa kama wachezaji wa kikosi cha pili kinachoundwa na vijana chini ya umri wa miaka 20, watakaokuwa wanakomazwa pia kikosi cha kwanza.
    Septemba mwaka huu Nkomola alisema amefaulu majaribio katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na atatakiwa kuanzia timu ya vijana hadi atakapofikisha umri wa miaka 18 Aprili mwakani ndipo atasaini mkataba rasmi na kuanza kuchezea timu ya wakubwa.
    Hata hivyo, wamiliki wa mchezaji huyo, Cambianso wameona bora ajiunge na Yanga kuliko kurejea  Etoile du Sahel.
    Tayari Nkomola ameanza kukomazwa kwenye timu ya wakubwa ya Tanzania na alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars ikitoa sare za 1-1 katika mechi zake mbili zilizopita dhidi ya Malawi Dar es Salaam na Benin mjini Coutonou.
    Na wakiwa kambini kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Malawi, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alimsifu kijana huyo na akamtabiria atafika mbali akiongeza juhudi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSHAMBULIAJI WA ETOILE DU SAHEL AJIUNGA NA YANGA SC MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top