• HABARI MPYA

  Friday, December 01, 2017

  REFA WA TANZANIA APENYA SEMINA YA CHAN 2018 MOROCCO

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Afrika limemteua refa Msaidizi, Frank John Komba wa Tanzania katika orodha ya marefa watakaopata mafunzo ya kuwania kuchezesha Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) inayotarajiwa kuanza Januari 13 hadi Februari 4 mwakani nchini Morocco.
  Komba ni refa msaidizi, maarufu kama mshika kibendera ambaye anakwenda kuwania kuchezesha fainali za pili mfululizo za Afrika, baada ya Mei mwaka huu kwenda Gabon kwenye fainali za U-17 za Afrika.
  Marefa wote 44 walioteuliwa wapo mjini Cairo, Misri tangu Novemba 27 hadi Desemba 1 kupata mafunzo maalum ya kuteua marefa wa kuchezesha mechi za fainali hizo zinazotarajiwa kupigwa katika miji ya Casablanca, Marrakech, Tangiers na Agadir.
  Frank John Komba (kulia) ni refa pekee wa Tanzania aliyeteuliwa kuchezesha CHAN mwakani 

  Marefa hao kutoka nchi 35 wanachama wa CAF, wanawania nafasi ya kuchezesha fainali za tano za CHAN zinazokutanisha wachezaji wanaocheza kwenye ligi za nchini mwao pekee na mafunzo yao ni ya nadharia na vitendo.

  Mafunzo mapya kwao yatakuwa ni matumizi ya Teknolojia ya picha za Video (VAR) kutoa maamuzi, mfumo ambao utafanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya CHAN mwakani.
  Meneja wa Marefa wa CAF, Eddy Maillet amesema kwamba marefa watakaochezesha fainali za Total CHAN Morocco 2018 watatajwa siku tano baada ya kozi hiyo.
  Kundi A linaundwa na wenyeji, Morocco, Guinea, Sudan na Mauritania, Kundi B kuna Ivory Coast, Zambia, Uganda na Namibia, Kundi C linaundwa na Libya, Nigeria, Rwanda na Equatorial Guinea na Kundi D lina timu za Angola, Cameroon, Kongo na Burkina Faso.
  Mechi ya ufunguzi na fainali zitafanyika kwenye Uwanja wa Mohamed V Complex mjini Casablanca, ambao pia ulitumika kwenye mchezo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2017.
  Wakati huo huo: Refa wa kike, Mtanzania Jonesia Rukyaa Kabakama kwa mara ya pili mfululizo ameteuliwa kuchezesha michuano ya Algarve Cup Februari hadi Machi mwakani nchini Ureno.
  Kabla ya kwenda Ureno, Jonesia anatarajiwa kushiriki semina maalumu iliyoandaliwa na FIFA itakayofanyika mjini Doha, Qatar kuanzia Februari 12- 16, mwakani.
  FAINALI zijazo za Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake zitafanyika nchini Ufaransa mwaka 2019. Algarve Cup ni michuano ya timu za taifa za wanawake ya kila mwaka inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Ureno (FPF) na imekuwa ikifanyika tangu mwaka 1994 nchini humo, ikiwa moja ya michauno mikongwe na ya muda mrefu ya wanawake. Bahati mbaya tu, michuano hiyo imekuwa haishirikishi timu za Afrika zaidi ya za Ulaya, Asia na Amerika pekee. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: REFA WA TANZANIA APENYA SEMINA YA CHAN 2018 MOROCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top