• HABARI MPYA

    Sunday, December 17, 2017

    KILA LA HERI ZANZIBAR HEROES…YAWANIA KOMBE LA CHELLENGE DHIDI YA HARAMBEE KENYA LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    ZANZIBAR inateremka kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos, Kenya jioni ya leo kumenyana na wenyeji, Kenya katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge. 
    Mchezo huo utakaoanza Saa 9:30 Alasiri, ukiufuatia wa kusaka mshindi wa tatu baina ya Burundi na Uganda utakaonza Saa 7:00 mchana, utaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV kupitia chaneli yake ya Azam Sports 2.  
    Huu ni mchezo wa pili katika michuano ya mwaka huu kuzikutanisha timu hizo, baada ya Desemba 9 katika mchezo wa Kundi A kutoka ya 0-0 Uwanja wa Kenyatta, Machakos pia.
    Lakini baada ya mchezo huo, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)  likaamuru wachezaji wa Zanzibar wakapimwe kama wametumia dawa za kuongeza nguvu – na hiyo ilitokana na kiwanho kizuri kilichoonyeshwa na timu hiyo.
    Kenya wamefika fainali baada ya kuitoa Burundi kwa bao 1-0 katika mchezo uliodumu kwa dakika 120 Alhamisi kufuatia timu hizo kutofungana ndani ya dakika 90, wakati Zanzibar wamewatoa mabingwa watetezi, Uganda kwa kuwachapa 2-1 ndani ya dakika 90 Ijumaa.
    Kenya iliongoza Kundi A lililokuwa na timu Tanzania Bara, Rwanda na Libya pia, ikifuatiwa na Zanzibar ambayo imekuwa katika kiwango kizuri mwaka huu, ikikumbushia mafanikio yake ya mwaka 1995 ilipochukua taji kwa mara ya kwanza nay a mwisho nchini Uganda, tena ikiwafunga wenyeji, The Cranes 1-0. 
    Mwaka huo, kikosi cha Zanzibar kilichocheza fainali kilikuwa; Riffat Said (marehemu), Nassor Salum ‘Cholo’, Hassan Ramadhan ‘Wembe’, Mohammed Shaaban ‘Kachumbari’, Shekha Khamis Rashid (Nahodha), Seif Khalfan, Said Mohamed ‘Makapu’, Victor John ‘Bambo’, Simai Hajji (marehemu), Juma Shekha/Abdulrahman Mohamed ‘Man’.
    Katika benchi walikuwapo makipa Mbarouk Suleiman na Salum Ali na akina wachezaji wa ndani akina Sabri Ramadhani ‘China’, Mbegu Mohammed, Nassri Nassor ‘Ndagi’, Issa Gazza na Udhia Abdallah.
    Mamia ya Wazanzibar waishio Kenya wamemiminika Machakos kuisapoti Zanziabr katika mchezo wa leo irudie kilichokifanya Uganda 1995.
    Kocha Mkuu alikuwa Hafidh Badru akisaidiwa na Shaaban Ramadhani, wakati Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) alikuwa Ali Ferej Tamim.
    Katika mchezo wa leo, kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ hatarajiiw kuwa na mabadiliko makubwa kutoka kikosi kilichowatoa mabingwa watetezi, Uganda katika Nusu Fainali – ni Mwinyi Hajji Mngwali pekee anayetarajiwa kuongezeka ambaye mchezo uliopita alikosekana kwa sababu alikuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano.  
    Kikosi cha Zanzibar leo kinatarajiwa kuwa; Mohammed Abulrahman Mohamed ‘Wawesha’, Ibrahim Mohamed, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah Kheri, Issa Haidari, Abdulaziz Makame, Mohamed Issa ‘Banka’, Mudathir Yahya, Ibrahim Hamad ‘Hilika’, Feisal Salum na Suleiman Kassim ‘Seleembe’.
    Mungu ibariki Zanzibar. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI ZANZIBAR HEROES…YAWANIA KOMBE LA CHELLENGE DHIDI YA HARAMBEE KENYA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top