• HABARI MPYA

    Friday, October 06, 2017

    MUWEKEZAJI SIMBA ANAWEZA KUTAJWA KESHO, KAMATI KUKUTANA NA WAANDISHI SERENA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI Maalum ya kusimamia mchakato wa zabuni ya kumpata mwekezaji kwenye muundo mpya wa klabu ya Simba kesho Saa 5:00 asubuhi inatarajiwa kukutana na Waandishi wa Habari 
    Tarifa ya Simba SC kwa vyombo vya Habari vya Habari iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu, Hajji Sunday Manara imesema kwamba mkutano huo utafanyika kwenye ukumbi wa Kivukoni 3 uliopo ndani ya hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam. 
    Kamati hiyo iliyoundwa mapema mwezi uliopita, ipo chinia ya Mwenyekitil, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Thomas Mihayo na Wajumbe wengine wanne, ambao ni Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan ‘Zungu’, Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Abdul-Razaq Badru, Wakili Dk. Damas Ndumbaro na Yusuph Maggid Nassor.
    Mohammed 'Mo' Dewji ndiye anapewa nafasi kubwa ya kuwa mmiliki wa klabu ya Simba

    Ikumbukwe Agosti 20, mwaka huu wanachama 1,216 wa klabu ya Simba waliridhia mfumo wa klabu yao kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC), Dar es Salaam.
    Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Jinsia na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala, Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Salim Abdallah 'Try Again' alisema kwamba asilimia 50 ya hisa zitauzwa kwa mwekezaji yeyote au wowote watakaoungana wasiozidi watatu, kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu hiyo. 
    Abdallah alisema mwekezaji huyo au hao, wanatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20 ili kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu, wakati kwa kuanzia wanachama wote wa Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa.
    Alisema asilimia nyingine 40 zitawekwa kama mtaji wa klabu na zitauzwa kwa wanachama baadaye, lakini wale wawekezaji walionunua asilimia 50 awali, hawataruhusiwa kununua hata hisa moja kwenye asilimia 40 za mtaji.
    Na baada ya mkutano wa huo, zoezi la  uhakiki wa wanachama wa ili kujua mgawanyo wa asilimia 10 za hisa utakavyokuwa – lilifuatia kabla ya kuundwa Kamati maalum ya kupitia maombi ya wawekezaji wanaotaka kununua asilimia 50 ya hisa.
    Kadhalika Simba iliendesha mikutano maalum katika mikoa kadhaa nchini kuwapa elimu ya mabadiliko wanachama wake. Na mfanyabiashara na mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kununua asilimia 50 ya hisa Simba.
    Tangu mwaka jana, Mo Dewji amekuwa akiisaidia uendeshwaji wa Simba kwa matarajio ya ndiye atakayepewa umiliki wa klabu katika mfumo mpya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MUWEKEZAJI SIMBA ANAWEZA KUTAJWA KESHO, KAMATI KUKUTANA NA WAANDISHI SERENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top