• HABARI MPYA

  Tuesday, May 09, 2017

  YANGA YARUDI TENA JUU LIGI KUU, YAWAPIGA WABABE WA SIMBA KAGERA SUGAR 2-1 TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na kwa ushindi huo, mabingwa hao watetezi wanafikisha pointi 62, sawa na Simba SC, lakini timu ya Jangwani wanapanda juu kwa wastani mzuri wa mabao na pia wana mchezo mmoja mkononi. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa msimu uliopita, Ngole Mwangole aliyesaidiwa na Mashaka Mwandembwa wa Mbeya pia na Silvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko kila timu ilikuwa imepata bao moja.
  Mabao ya Simon Msuva (kulia) na Obrey Chirwa (kushoto) leo yameirudisha juu Yanga katika Ligi Kuu
  Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa akimtoka beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi
  Winga wa Yanga, Geoffrey Mwashiuya akiruka 'kwanja' la beki wa Kagera Sugar, Geoffrey Taita 
  Kiungo wa Kagera Sugar, Ame Ali 'Zungu' akipasua katikati ya Amissi Tambwe (kulia) na Haruna Niyonzima (kushoto)
  Mbaraka Yussuf akimchambua kipa wa Yanga, Benno Kakolanya baada ya kumuacha beki Kevin Yondan (nyuma)

  Yanga SC ndiyo waliotangulia kwa bao la winga Simon Happygod Msuva dakika ya 38 kabla ya Kagera Sugar kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wake, Mbaraka Yussuf Abeid dakika ya 45.
  Msuva alifunga bao lake la 13 msimju huu akimalizia kona nzuri iliyopigwa na winga wa kushoto, Geoffrey Mwashiuya, wakati Mbaraka alifunga bao lake la 12 msimu huu baada ya kufanikiwa kumzidi maarifa beki wa Yanga, Kevin Yondan wakati wakiwania krosi ya juu ya Edward Christipher na kwenda kumchambua kipa Benno Kakolanya.
  Kipindi cha pili, Yanga walikianza vizuri tena na kufanikiwa kupata bao la pili na la ushindi dakika ya 52 kupitia mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyemalizia krosi ya kiungo fundi, Haruna Niyozima.
  Mchezo ulizidi kuwa wa kupendeza baada ya bao hilo, kwani Yanga waliongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la tatu, huku Kagera Sugar wakisaka bao la kusawazisha.
  Mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe haikuwa bahati yake leo kumfunga ‘Tanzania One’ wa zamani, Juma Kaseja baada ya kupoteza nafasi tatu za wazi.
  Na ikawa siku mbaya zaidi kwa Kagera Sugar, baada ya mshambuliaji wake tegemeo, Mbaraka Yussuf Abeid kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 87 baada ya kumchezea rafu beki wa Yanga, Kevin Yondan.
  Pamoja na Kagera kucheza pungufu kuanzia hapo, lakini wakafanikiwa kumaliza mchezo bila kuongezwa bao.  
  Kikosi cha Yanga SC; Benno Kakolanya, Hassan Kessy/Juma Abdul dk62, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Obrey Chirwa/Matheo Anthony dk77 na Geoffrey Mwashiuya/Geoffrey Mwashiuya dk83.
  Kagera Sugar; Juma Kaseja, Godfrey Taita/Themi Felix dk72, Mwaita Gereza, Babu Ali Seif/Anthony Matogolo dk57, Mohammed Fakhi, George Kavilla, Suleiman Mangoma, Ally Nassor ‘Ufudu’, Mbaraka Yussuf, Ame Ali ‘Zungu’ na Edward Christopher/Japhet Makalao dk62.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YARUDI TENA JUU LIGI KUU, YAWAPIGA WABABE WA SIMBA KAGERA SUGAR 2-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top