• HABARI MPYA

    Sunday, May 28, 2017

    MKUDE APATA AJALI MBAYA DUMILA, MMOJA AFARIKI DUNIA...WENGINE HALI MBAYA

    Na Mahmoud Zubeiry, DUMILA
    NAHODHA wa Simba, Jonas Mkude amenusurika katika ajali mbaya ya gari iliyotokea eneo la Dumila mkoani Morogoro mchana wa leo.
    Mkude na watu wengine watano akiwemo dereva walikuwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 wakisafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
    Na walipofika Dumila tairi la mbele likapasuka na gari hiyo kupoteza mwelekeo hadi kwenye pori upande wa kushoto.
    Abiria mmoja aliyatajwa kwa jina la Shose Fidelis amefariki dunia, wakati wengine Jasmin na Faudhia wamelazwa hospitali ya mkoa wa Morogoro na hali zao ni mbaya.
    Mkude amerejeshwa Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi, wakati ereva ambaye pia ndiye mmiliki wa gari ajulikanaye kwa jina la utani, Rais wa Kibamba yupo chini ya uangalizi wa Polisi.
    Wanachama wa Simba waliokuwa kwenye basi dogo wakirejea Dar es Salaam walipofika eneo la tukio walisimama kutoa msaada. 
    Gari ya aina Toyota Land Cruiser V8 ambalo alikuwemo Mkude baada ya kupata ajali
    Mkude aliisaidia Simba jana kubeba Kombe la ASFC kwa kuifunga Mbao 2-1 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma

    Mkude alikuwa anatoka Dodoma, ambako jana aliisaidia Simba kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Katika fainali kali na ya kusisimua ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na mabao matatu yakapatikana katika dakika 30 za nyongeza, Simba mawili, Mbao moja.
    Wachezaji Frederick Blagnon raia wa Ivory Coast na Robert Ndaki ambao wote walitokea benchi kipindi cha pili ndiyo waliokwenda kuzifungia mfululizo timu zao.
    Blagnon alianza kuwainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 95 baada ya kumzidi maarifa beki wa Mbao FC kufuatia pasi ndefu ya beki wa kushoto pia, Abdi Banda.
    Lakini Ndaki akaisawazishia Mbao dakika ya 109 akitumia makosa ya Banda aliyezubaa akidhani mfungaji kaotea.
    Wakati wengi wanaamini mchezo utaamuliwa kwa mikwaju ya penalti, lakini refa Ahmed Kikumbo akawazawadia Simba penalti baada ya beki mmoja wa Mbao FC kuunawa mpira uliopigwa na Abdi Banda dakika 119.
    Wachezaji wa Mbao FC walimzonga refa huyo kabla ya kuamua kutulia na kukubali mchezo uendelee, ndipo winga Shiza Ramadhan Kichuya akaenda kuifungia Simba bao la ushindi na kuamsha shangwe na nderemo Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Askari wa usalama barabarani akiangalia gari hilo baada ya kupindukia porini
    Wanachama wa Simba waliokuwa kwenye basi dogo wakirejea Dar es Salaam walipofika eneo la tukio walisimama kutoa msaada 
    Wamachama wa Simba wakilitazama gari lililombeba Nahodha wao baada ya ajali
    Wapenzi wa Simba wakiwa wametahayari eneo la tukio na chini ni Mwandishi wa Habari, Mwani Nyangassa akielekea eneo la tukio 

    Wakati kikosi cha Simba kimebaki Dodoma kwa ajili ya kwenda kuonyesha Kombe lao Bungeni kesho na baadaye kwenda kucheza mechi ya kirafiki Singida, Mkude na wachezaji wengine wa Simba walioitwa timu ya taifa wamelazimika kuondoka leo kwa usafiri tofauti kurejea Dar es Salaam kujiunga na Taifa Stars.
    Mkude aliomba lifti kwa rafiki yake, Rais wa Kibamba wakati wengine akiwemo beki Abdi Banda walipanda mabasi. Wengine walioitwa Taifa Stars kutoka Simba ni beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, viungo Said Ndemla, Kichuya, Muzamil Yassin, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na mshambuliaji Ibrahim Hajib.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKUDE APATA AJALI MBAYA DUMILA, MMOJA AFARIKI DUNIA...WENGINE HALI MBAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top