• HABARI MPYA

    Saturday, May 27, 2017

    BECKHAM AWASILI DAR NA FAMILIA YAKE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa zamani wa England, David Robert Joseph Beckham leo ametua Tanzania akiwa na familia yake, mkewe, Victoria Adams ‘Posh’ na wanawe, Brooklyn Joseph, Romeo James, Cruz David na Harper Seven.
    Beckham, kiungo wa zamani wa Manchester United, Preston North End, Real Madrid, AC Milan, LA Galaxy na Paris Saint-Germain ameonekana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwasili na familia yake leo.
    Hata hivyo, Bekcham hakutaka kuzungumza chochote juu ya ujio wake na alipotoka nje alipokewa na wenyeji wake, moja kwa moja kuelekea kwenye gari na kutokomea kusikojulikana, ingawa ni katikati ya mji.
    David Beckham wakati akitoka nje ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam leo baada ya kuwasili 

    Beckham anajivunia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa England kushinda mataji ya Ligi Kuu za nchi nne; England, Hispania, Marekani na Ufaransa kabla ya kustaafu soka Mei 2013 baada ya miaka 20 ya kuwa uwanjani na kushinda mataji 19.
    Akiwa anafahamika kwa utoaji wake wa pasi nzuri na kupiga vizuri mipira iliyokufa enzi zake akicheza wingi ya kulia, Beckham alishika nafasi ya pili mara mbili katika tuzo ya Mwanasoka Bpra wa Dunia, maarufu kama Ballon d'Or.
    Kisoka, Beckham aliibukia Manchester United, ambako alianza kuchezea kikosi cha kwanza mwaka 1992 akiwa ana umri wa miaka 17 na akafanikiwa kushinda mataji sita ya Ligi Kuu yaa timu hiyo na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999.
    Baada ya hapo akaenda kucheza kwa misimu minne Real Madrid, akishinda taji la La Liga katika msimu wake wa mwisho na klabu hiyo.
    Julai mwaka 2007 akasaini mkataba wa miaka mitano na LA Galaxy ya Marekani na akiwa huko, akaenda kucheza kwa mkopo Italia mara mbili mwaka 2009 na 2010. Na piaanajivunia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Muingereza kucheza mechi 100 za Ligi ya Mabingwa.
    Kwenye soka ya kimataifa, Beckham aliichezea kwa mara ya kwanza England Septemba 1, mwaka 1996 akiwa ana umri wa miaka 21 kabla ya kuwa Nahodha kwa miaka sita akicheza jumla ya mechi 58 zikiwemo za Kombe la Dunia 1998, 2002 na 2006, na fainali mbili za Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2000 na 2004.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BECKHAM AWASILI DAR NA FAMILIA YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top