• HABARI MPYA

    Monday, May 29, 2017

    NI MALI WAFALME WA SOKA YA VIJANA AFRIKA TENA

    HISTORIA imewekwa jana jana kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 nchini Gabon 2017, wakati Mali ilipokuwa nchi ya kwanza kutwaa taji mara mbili mfululizo, kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Black Starlets ya Ghana. 
    Katika mchezo mzuri wa fainali uliofanyika Uwanja wa d'Angondjé au l'Amitie kama unavyofahamika pia Mamadou Samake ndiye aliyefunga bao pekee dakika ya 22 akimalizia mpira uliookolewa na kipa wa Ghana, baada ya mkwaju wa penalti wa Seme Camara na Mali inaungana na nchi kama Nigeria, Ghana na Gambia zilizotwaa taji hilo mara mbili kila moja tangu mwaka 1995 ilipoanzishwa michuano hiyo.
    Mchezo ulikuwa mkali tangu mwanzo na timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu, lakini washambuliaji pacha wa Mali, Seme Camara na Hadji Drame waliipa wakati mgumu mno safu ya ulinzi ya Ghana.
    Dakika ya 30 Mali walipata penalti nyingine, lakini kipa wa Black Starlets, Danlad Ibrahim akapangua mkwaju wa Mamadou Samake na mwisho wa mchezo, Nahodha wa mabingwa, Mohammed Camara akatajwa Mchezaji Bora wa Mechi.
    Mabingwa Mali kwa pamoja na washindi wa pili, Ghana, washindi wa tatu Guinea na Niger walioshika nafasi ya nne, wataiwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia la FIFA la U-17 nchini India mwezi Oktoba.
    Mapema katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, Guinea iliifunga Niger 3-1 na kumalia nyuma ya Ghana.  Mabao ya Guinea yamefungwa na mshambuliaji Djibril Fandje Toure mawili moja kila kipindi na Eldadj Abdourahamane Bah, wakati la Niger lilifungwa na Ibrahim Boubacar Marou.
    Michuano hiyo, ilishirikisha timu nane kuanzia ngazi ya makundi, Kundi A likiundwa na Gabon, Ghana, Guinea na Cameroon, wakati Kundi B liliundwa na Angola, Niger, Mali na Tanzania iliyokuwa inashiriki kwa mara ya kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI MALI WAFALME WA SOKA YA VIJANA AFRIKA TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top