• HABARI MPYA

    Saturday, May 27, 2017

    SIMBA YAREJEA ANGA ZA KIMATAIFA, YAIGONGA MBAO 2-1 NA KUTWAA KOMBE LA AZAM

    Na Mahmoud Zubeiry, DODOMA
    SIMBA SC imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Katika fainali kali na ya kusisimua ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na mabao matatu yakapatikana katika dakika 30 za nyongeza, Simba mawili, Mbao moja.
    Wachezaji Frederick Blagnon raia wa Ivory Coast na Robert Ndaki ambao wote walitokea benchi kipindi cha pili ndiyo waliokwenda kuzifungia mfululizo timu zao.
    Wachezaji wa Simba SC wakifurahia na Kombe lao baada ya kukabidhiwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma leo
    Mfungaji wa bao la ushindi la Simba, Shiza Kichuya akimtoka beki wa Mbao leo 
    Mfungaji wa bao la kwanza la Simba, Frederick Blagnon (katikati) akipambana na wachezaji wa Mbao FC
    Beki wa Simba, Mgahan James Kotei aliyeibua Mchezaji Bora wa Mechi akimdhibiti mshambuliaji wa Mbao FC, George Sangija  
    Mshambuliaji wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo akivuta mguu kufumua shuti dhidi ya wachezaji wa Mbao

    Blagnon alianza kuwainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 95 baada ya kumzidi maarifa beki wa Mbao FC kufuatia pasi ndefu ya beki wa kushoto pia, Abdi Banda.
    Lakini Ndaki akaisawazishia Mbao dakika ya 109 akitumia makosa ya Banda aliyezubaa akidhani mfungaji kaotea.
    Wakati wengi wanaamini mchezo utaamuliwa kwa mikwaju ya penalti, lakini refa Ahmed Kikumbo akawazawadia Simba penalti baada ya beki mmoja wa Mbao FC kuunawa mpira uliopigwa na Abdi Banda dakika 119.
    Wachezaji wa Mbao FC walimzonga refa huyo kabla ya kuamua kutulia na kukubali mchezo uendelee, ndipo winga Shiza Ramadhan Kichuya akaenda kuifungia Simba bao la ushindi na kuamsha shangwe na nderemo Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Kiungo Mghana wa Simba, James Kotei ambaye sasa anatumika kama beki wa kati ndiye ameibuka Mchezaji Bora wa Mechi ya leo, wakati mfungaji bora wa mashindano ni Mzambia, Obrey Chirwa wa Yanga.
    Simba imekata tiketi ya kurejea kwenye michuano ya Afrika baada ya kuikosa kwa miaka minne na mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akaenda kuwakabidhi taji lao Wekundu wa Msimbazi.         
    Kilichofuata ni shangwe za wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba kuelekea kwenye mitaa ya mji wa Dodoma, kabla ya kesho asubuhi kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam na Kombe lao.
    Kikosi cha Simba kilikuwa; Daniel Agyei, Janvier Besala Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tahabalala’/Abdi Banda dk51, James Kotei, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Said Ndemla/Frederick Blagnon dk80 na Juma Luizio/Ibrahim Hajib dk60.
    Mbao: Benedict Haule, Asante Kwasi, Yussuf Ndikumana, David Mwasa, Salmin Hozza, Boniface Maganga, George Sangija/Dickson Ambundo dk59/Rajesh Kotecha dk104, Jamal Mwambeleko, Pius Buswita, Habib Hajji/Robert Ndaki dk104 na Ibrahim Njohole.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAREJEA ANGA ZA KIMATAIFA, YAIGONGA MBAO 2-1 NA KUTWAA KOMBE LA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top