• HABARI MPYA

    Tuesday, May 23, 2017

    MANJI AJIONDOA RASMI YANGA BAADA YA MIAKA 11

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Yanga SC, Yussuf Manji amethibitisha kujiuzulu Uenyekiti wa klabu hiyo kuanzia juzi na kumuachia Makamu wake, Clement Sanga akaimu.
    “Ni taarifa yangu na inajieleza yenyewe,”amesema Manji akizungumza kuthibitisha barua inayosambazwa kama taarifa kwa vyombo vya Habari.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Na Manji anaondoka Yanga wakati tayari klabu imepata udhamini wa kampuni ya SportPesa, jambo ambalo halitaifanya iyumbe kiuchumi.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji atakumbukwa kwa mengi – kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka huu, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Hali hiyo ilisababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ya kiufadhili Yanga na kufanya wachezaji wakose mishahara kwa kipindi chote hicho kabla ya viongozi wenzake kuanza kufanya jitihada za kulipa taratibu.
    Lakini kwa ujumla ni udhamini wa SportPesa ndiyo unakuwa mkombozi wa tatizo la kiuchumi la Yanga baada ya Manji kuondoka. 


     

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI AJIONDOA RASMI YANGA BAADA YA MIAKA 11 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top