• HABARI MPYA

    Sunday, May 28, 2017

    HONGERA SIMBA SC, USAJILI SASA UFANYWE NA BENCHI LA UFUNDI

    MWAKANI Simba SC itacheza tena michuano ya Afrika baada ya kuikosa kwa miaka minne. 
    Hiyo inafuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya timu ngumu, Mbao FC ya Mwanza katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) jana Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Na baada ya kuzidiwa kete ‘dakika za mwisho’ na mahasimu wao, Yanga SC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara waliojikatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo, mwakani – Simba jana wamepoza machungu. 
    Simba ilicheza michuano ya Afrika kwa mara ya mwisho mwaka 2013 na kutolewa na Recreativo de Lobolo ya Angola kwa vipigo vya nyumbani na ugenini, ikifungwa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na 4-0 ugenini.
    Tangu hapo, Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakizishuhudia Azam na Yanga zikibadilisha ndege kwenda nchi mbalimbali kwa michuano ya Afrika.
    Katika mchezo wa jana na Mbao FC, dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na mabao matatu yakapatikana katika dakika 30 za nyongeza, Simba mawili, Mbao moja.
    Wachezaji Frederick Blagnon raia wa Ivory Coast na Robert Ndaki ambao wote walitokea benchi kipindi cha pili ndiyo waliokwenda kuzifungia mfululizo timu zao.
    Blagnon alianza kuwainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 95 baada ya kumzidi maarifa beki wa Mbao FC kufuatia pasi ndefu ya beki wa kushoto pia, Abdi Banda.
    Lakini Ndaki akaisawazishia Mbao dakika ya 109 akitumia makosa ya Banda aliyezubaa akidhani mfungaji kaotea.
    Wakati wengi wanaamini mchezo utaamuliwa kwa mikwaju ya penalti, lakini refa Ahmed Kikumbo akawazawadia Simba penalti baada ya beki mmoja wa Mbao FC kuunawa mpira uliopigwa na Abdi Banda dakika 119.
    Wachezaji wa Mbao FC walimzonga refa huyo kabla ya kuamua kutulia na kukubali mchezo uendelee, ndipo winga Shiza Ramadhan Kichuya akaenda kuifungia Simba bao la ushindi na kuamsha shangwe na nderemo Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akaenda kuwakabidhi taji lao Wekundu wa Msimbazi na baada ya hapo shangwe za wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba zikafuatia kuelekea kwenye mitaa ya mji wa Dodoma, kabla ya leo asubuhi kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam na Kombe lao.
    Hakika ushindi huo ni faraja kwa wana Simba wote, kuanzia wachezaji, benchi la Ufundi, viongozi, wanachama na mashabiki wake.
    Ni ushindi ambao wameutafuta kwa miaka mitano iliyopita, wakibadilisha makocha na wachezaji bila mafanikio hadi jana walipotimiza azma yao.
    Na haukuwa ushindi mwepesi, kwani walikutana na timu ngumu iliyowaweka roho juu kwa muda wote wa mchezo na furaha kamili ilianza baada ya filimbi ya mwisho.
    Ni kwa sababu zote hizo, Simba wanastahili kupewa pongezi – kwani kile walichokuwa wakikipigania kwa muda mrefu, tiketi ya michuano ya Afrika wamekipata jana.
    Ushindi wa Kombe la TFF ni nafasi ya kucheza michuano ya Afrika na bila shaka Simba wanalitambua hilo na wanajua nini kinafuata mbele yao.
    Maana yake ni wakati sasa wa kuanza kujiandaa kwa michuano hiyo, kwa kuhakikisha wanapitia vizuri taarifa ya benchi la ufundi chini ya kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Omog na kuifanyia kazi.
    Wazi taarifa ya Omog haitakosa mapendekezo ya uimarishaji wa kikosi kwa kusajili wachezaji wa nafasi mbalimbali, lakini itapendeza ukawa usajili ambao umetokana na taarifa ya benchi la Ufundi na si utashi wa kiongozi, au viongozi.
    Kwa kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu na kutwaa Kombe la TFF ni kielelezo tosha kwamba Simba ni bora dhidi ya timu nyngine, ukiondoa mabingwa wa nchi, Yanga. 
    Hivyo Simba haihitaji kubomolewa, bali inahitaji kuimarishwa kwa kuongezewa wachezaji wachache kulingana na mapendekezo ya benchi la Ufundi. Hongera Simba SC.      
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HONGERA SIMBA SC, USAJILI SASA UFANYWE NA BENCHI LA UFUNDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top