• HABARI MPYA

  Monday, May 01, 2017

  YANGA WAMCHONGEA RAIS WA SIMBA AVEVA TFF, WASEMA ANATAKA KUVURUGA AMANI KATIKA SOKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAMACHAMA watano wa klabu ya Yanga wameandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumchongea Rais wa Simba, Evans Elieza Aveva achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo cha kuitisha maandamano ya wanachama ya klabu yake.
  Wanachama hao Jumanne Zegege, Hamisi Ramadhani, Waziri Jitu, Said Ngota na Nasra Ulembo katika barua yao kwenda kwa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa wamesema Aveva aliandika barua na kuweka saini yake kuipeleka kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Simon Sirro akiomba kibali cha kufanya maandamano.
  Yanga wanataka Rais wa Simba, Evans Aveva (kulia) achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuitisha maandamano

  Wamesema kitendo alichofanya Aveva kilikuwa ni cha uchochezi na chenye kuhatarisha amani na pia ni kosa kisheria kupeleka masuala ya soka kwenye vyombo vya dola, hivyo wanaiomba Sekretarieti ya TFF impeleke Aveva Kamati ya Maadili.
  Hata hivyo, maandamano hayo hayakufanyika baada ya Aveva mwenyewe kutangaza kuyasitisha kufuatia tamko la Serikali kuikutanisha klabu hiyo na TFF wamalize tofauti zao.
  Pamoja na hayo, wanachama hao wamerudi nyuma kwenye sakata la mchezaji Mohammed Fakhi kudaiwa kuichezea Kagera Sugar dhidi ya timu yake ya zamani, Simba SC Aprili 2, mwaka huu akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
  Ikumbukwe katika sakata hilo, awali Simba iliyofungwa 2-1 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ilipewa pointi tatu na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72, kabla ya kupokonywa na Kamati ya Sheria Katiba na Hadhi za Wachezaji nakurejeshewa Kagera Sugar.
  Kamati ya Saa 72 ilijiridhisha Fakhi alikuwa ana kadi tatu za njano ndiyo maana ikaipokonya Kagera Sugar ushindi, lakini Kamati ya Sheria Katiba na Hadhi za Wachezaji ilidai rufaa ya Simba ilikatwa nje muda wa kisheria na haikulipiwa ada hivyo haikustahili hata kusikilizwa na maana yake kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kilichotoa maamuzi hayo kilikuwa batili.
  Lakini katika barua yao kwenda kwa Mwesigwa, wanachama hao wamesema kwamba mambo mengi yameripotiwa kwenye vyombo vya Habari ikiwemo taarifa za refa, washika vibendera, refa wa akiba na Kamisaa kutofautiana juu ya Fakhi kuonyeshwa au kutoonyeshwa kadi ya tatu ya njano katika mchezo dhidi ya African Lyon Januari 18, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba.
  “Hii ni wazi kuwa sakata hili limegubikwa na rushwa na linatoa dalili za kupanga matokeo, Katibu Mkuu tunakutaka uchukue hatua kwa mujibu wa kanuni za Maadili za TFF ili wahusikawakiwemo viongozi na waamuzi wafungiwe maisha,”wamesema wanachama hao katika barua yao.
  Pamoja na hayo, wameitaka Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji kuweka hadharani taarifa kamili ya uchunguzi wao katika kesi ya Fakhi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAMCHONGEA RAIS WA SIMBA AVEVA TFF, WASEMA ANATAKA KUVURUGA AMANI KATIKA SOKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top