• HABARI MPYA

    Wednesday, May 10, 2017

    YANGA NA MBEYA CITY SASA KUCHEZWA ‘USIKU’ TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji, Yanga SC na Mbeya City ya Mbeya uatafanyika kama kawaida Jumamosi ya Mei 13, lakini kuanzia Saa 12:00 jioni, badala ya Saa 10:00.
    Taarifa ya Yanga SC jioni ya leo imesema kwamba mchezo huo umesogezwa mbele muda wa kuanza katika kujaribu kuwapa fursa watu wengi waushuhudie baada ya mizunguko yao ya kutwa ya kujitafutia riziki.
    “Maamuzi haya yamezingatia matakwa na masilahi ya wadau wa soka nchini ambao wana kiu na hamu ya kuutazama mchezo huo, lakini pia wakiwa ni sehemu ya wadau wa mchezo wa riadha utakayofanyika Uwanja wa Taifa Jumamosi hiyo hiyo,”imesema taarifa ya Yanga. 
    Yanga jana iliifunga Kagera Sugar 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

    Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kurejea kileleni mwa Ligi Kuu baada ya ushindi wa mabao 2-1 jana dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba Uwanja wa Taifa.
    Na kwa ushindi huo, mabingwa hao watetezi wanafikisha pointi 62, sawa na Simba SC, lakini timu ya Jangwani inapanda juu kwa wastani mzuri wa mabao na pia wana mchezo mmoja mkononi. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa msimu uliopita, Ngole Mwangole aliyesaidiwa na Mashaka Mwandembwa wa Mbeya pia na Silvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko kila timu ilikuwa imepata bao moja.
    Yanga SC ndiyo waliotangulia kwa bao la winga Simon Happygod Msuva dakika ya 38 kabla ya Kagera Sugar kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wake, Mbaraka Yussuf Abeid dakika ya 45.
    Msuva alifunga bao lake la 13 msimju huu akimalizia kona nzuri iliyopigwa na winga wa kushoto, Geoffrey Mwashiuya, wakati Mbaraka alifunga bao lake la 12 msimu huu baada ya kufanikiwa kumzidi maarifa beki wa Yanga, Kevin Yondan wakati wakiwania krosi ya juu ya Edward Christipher na kwenda kumchambua kipa Benno Kakolanya.
    Kipindi cha pili, Yanga walikianza vizuri tena na kufanikiwa kupata bao la pili na la ushindi dakika ya 52 kupitia mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyemalizia krosi ya kiungo fundi, Haruna Niyozima.
    Na ikawa siku mbaya zaidi kwa Kagera Sugar, baada ya mshambuliaji wake tegemeo, Mbaraka Yussuf Abeid kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 87 baada ya kumchezea rafu beki wa Yanga, Kevin Yondan. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA NA MBEYA CITY SASA KUCHEZWA ‘USIKU’ TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top