• HABARI MPYA

  Wednesday, May 03, 2017

  SAKATA LA FAKHI...SIMBA WATAKA KUPELEKA KESI FIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba imesema kwamba itapeleka malalamiko Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baada ya kupokwa pointi tatu na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Simba ilinyang’amywa pointi hizo ilizopewa na Kamati ya Masaa 72 ya TFF kufuatia timu ya Kagera kumchezesha Mohammed Fakhi, akidaiwa kuwa na kadi tatu za njano katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika mjini Bukoba.
  Rais wa Simba, Evans Aveva akizungumza na Waandishi wa Habari leo Dar es Salaam

  Katika mchezo huo Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 ambapo baadaye waliamua kupeleka malalamiko yao TFF kwamba mchezaji huyo alikuwa na kadi tatu za njano.
  Baadaye Kamati ya Saa 72 ilikaa na kupitia nyaraka mbalimbali kuhusu suala hilo ambapo ilitoa maamuzi kwamba Kagera Sugar wapokonywe pointi tatu na mabao matatu kufuatia kosa hilo ambazo moja kwa moja zilipekwa katika timu ya Simba.
  Baada ya kupita siku chache Kagera Sugar ilikata rufaa kwa kuomba hukumu hiyo ipitiwe upya ambapo Kamati ya Sheria ilikutana na kuwaita waamuzi wa mchezo, mchezaji husika aliyekuwa akilalamikiwa na viongozi wa timu zote mbili ambao walifanya nao mahojiano.
  Suala hilo lilileta utata mkubwa na kuifanya Kamati ya Sheria kuchukua muda mrefu kulikamilisha ambapo baadaye walitoa maamuzi kwamba kuna makosa yalifanyika na kwamba pointi walizopokwa Kagera, warudhiwe.
  Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa Simba, Evance Aveva, alisema kwamba walifanya uchunguzi wa kina kuhusu suala la Fakhi na kubaini alikuwa ana kadi tatu za njano.
  Alisema kuwa awali walipewa haki yao lakini baadaye iliyeyuka kufuatia Kamati ya Sheria kutengua hukumu ambayo ilitolewa na Kamati ya Saa 72.
  Alisema kuwa kwa sasa wanasubiri barua kutoa TFF ambayo itawapa mwongozo kwamba wamenyang’anywa pointi hizo kwa kanuni ipi ili wapige hatua mbele zaidi kutafuta haki yao.
  “Ni suala la kushangaza na tukikaa kimya hatuwezi kupaya haki yetu, tulitoa malalamiko TFF kwamba tumebaini Fakhi alichezeshwa akiwa na kadi tatu za njano na kupewa pointi tatu na mabao matatu.
  “Lakini cha kushangaza Kamati ya Sheria ilikaa kupitia upya hukumu ambao hawakuitoa wao na kutoa maamuzi ambayo hayastahili, tunasubiri barua ya TFF ili tuchukue hatua zaidi,” alisema Aveva.
  Aveva alisema kwamba wameshafanya mawasiliano na kitengo cha masuala ya rufaa cha kilichopo chini ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na kupata mwongozo juu ya kukata rufaa.
  Alisema kuwa uongozi wa Simba umeamua kulipeleka suala hilo FIFA, ili kupewa haki yao.
  Aidha Aveva alisema kwamba wamefanya uchunguzi wa njia ya kukata rufaa FIFA ambapo ghara yake itakuwa dola 15,000 ili suala lao liweze kusikilizwa na kutolewa ufafanuzi.
  Alisema kwamba Kamati ya Sheria haikuwa na haki ya kutengua hukumu iliyotolewa awali kwani na kutoa visingizio ambavyo vipo nje ya kanuni za mchezo wa soka.
  “Suala letu tunalipeleka FIFA, tumeshapewa mwongozo na CAF na kwamba gharama zake zitakuwa dola 15,000 na kwamba tumeamua kwenda ngazi za juu ili haki ipatikane.
  “Kamati ya Sheria imekuja na majibu ambayo yapo nje ya kanuni kwamba tulichelewa kulipa gharama za malalamiko na suala la kumshirikisha mjumbe ambaye hakustahili, kitu ambacho sio sahihi, tunataka kujua kanuni zipi zilizotumika kutoa adhabu na ile iliyotumika kuiondoa,” alisema Aveva.
  Alisema kwamba mashabiki wa Simba wanatakiwa kuwa watulivu kwa sasa na kwamba hatua uongozi utakaochukua itaanza mara moja baada ya kupata barua kutoka TFF.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAKATA LA FAKHI...SIMBA WATAKA KUPELEKA KESI FIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top