• HABARI MPYA

  Wednesday, May 03, 2017

  MAKAMU WA RAIS TFF ASEMA JKT RUVU ILIAMUA KWENDA KUFIA TANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kwamba JKT Ruvu ilihamia Tanga ikiwa tayari ipo katika hatari ya kushuka Daraja na mkoa huo haustahili lawama yoyote timu hiyo ikishuka.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana katika mahojiano maalum ofisi za TFF, Dar es Salaam, Karia amesema kwamba kushuka kwa JKT Ruvu hakufanani za timu za Tanga, JKT Mgambo, Coastal Union na African Sports zilizoteremka kwa pamoja msimu uliopita.
  Karia ameifananisha JKT Ruvu na mgonjwa aliyetolewa hospitali moja akiwa tayari ana hali mbaya na kuhamishiwa hospitali nyingine kwa matarajio ya kupata ahueni, lakini ikashindikana.
  Hassan Dilunga wa JKT Ruvu (kushoto) akimfuatilia Mzimbabwe Thabani Kamusoko wa Yanga (kulia)


  Karia, mdau mkubwa wa soka Tanga, amerudi nyuma na kusema si kweli mkoa wa Tanga una gundu la kushusha timu Daraja, kwani hata JKT Ruvu ilipanda Ligi Kuu kutoka kituo cha mkoa huo zaidi ya miaka 15 iliyopita.
  “JKT Ruvu imeenda (Tanga) bado mechi chache sana kwa hatua ya kumaliza Ligi Kuu, lakini imemaliza raundi ya kwanza pia iko chini, kwa hiyo naweza kusema ni sawasawa na mgonjwa aliyekuwa anahudumiwa Ilala, akaamua aende akafie Muhimbili,”alisema, Karia ambaye ni kiongozi wa zamani wa Coastal Union.
  Karia ambaye pia ni kiongozi wa zamani wa Chama cha Soka Tanga amesema hata lawama za kwamba mkoa huo uliishusha pia Twiga SC ya Kinondoni iliyokuwa inamilikiwa na Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Iddi Azzan haina mashiko.
  “Azzan aliileta Twiga Tanga mechi za mwisho baada ya kuanza kuona kwamba labda Dar es Salaam inapigwa vita akaileta pale, kwa hiyo inaonyesha jinsi gani ambavyo Tanga watu wanapenda mpira,”alisema. 
  JKT Ruvu inashika mkia katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoshirikisha timu 16 kwa pointi zake 23 za mechi 27, juu yake kuna Maji Maji ya Songea yenye pointi 26 za mechi 27, ambayo nayo ipo nyuma ya Toto Africans ya Mwanza yenye pointi 26 za mechi 26.
  Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa nchini imekuwa moja ya timu za ushindani katika Ligi Kuu tangu ilipopanda mwaka 2002, lakini msimu huu inalekea kabisa kuipa mkono wa kwaheri ligi hiyo. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAKAMU WA RAIS TFF ASEMA JKT RUVU ILIAMUA KWENDA KUFIA TANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top