• HABARI MPYA

    Thursday, May 04, 2017

    MALINZI: SERENGETI BOYS IMEIVA KWA FAINALI ZA AFRIKA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kwamba mechi saba za kujipima nguvu walizopata timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys zinatosha kabisa kabla ya kuingia kwenye Fainali za Afrika nchini Gabon wiki ijayo.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mchana, Malinzi amesema kwamba anaamini mechi saba zimetosha kabisa kwa benchi la ufundi la timu hiyo kuiweka sawa timu yao kabla ya kuingia kwenye fainali hizo.
    “Tunaamini hizi mechi saba hizi na kwa mujibu wa programu ya walimu waliyokuwa nayo kwamba zinawatosha kwa ajili ya kuwatengenezea utimamu wa mwili na kwa ajili ya kuwajengea kujiamini, kwa hiyo tarehe saba sasa, timu itaingia rasmi nchini Gabon kwenye mji wa Libreville,”amesema. 
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi (kulia) amesema Serengeti Boys imeiva kwa Fainali za Afrika nchini Gabon



    Serengeti Boys jana imekamilisha mechi zake za kujipima nguvu za kujiandaa AFCON ya U-17 nchini Gabon michauno inayotarajiwa kuanza Mei 14 hadi 28 kwa kufungwa 1-0 na wenyeji Cameroon mjini Yaounde.
    Kipigo hicho ni sawa na kisasi, baada ya Serengeti Boys kuifunga Cameroon 1-0 Aprili 30, mwaka huu katika mchezo mwingine wa kujipima nguvu.
    Siku hiyo, bao la Serengeti Boys lilifungwa na Ally Ng'anzi dakika ya 36 katika mchezo ambao ulihudhuriwa na gwiji wa soka wa Cameroon, Rogger Milla.
    Serengeti Boys ilitua Younde, Cameroon Alhamisi iliyopita ikitokea mjini Rabat, Morocco ambako iliweka kambi ya karibu mwezi mmoja na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Gabon na kushinda 2-1 kila mchezo.
    Kwa ujumla Serengeti Boys imekwishacheza mechi saba tangu kuanza kambi rasmi ya maandalizi fainali za Gabon, baada ya awali kuifunga Burundi mara mbili, Machi 30 mabao 3-0 na Aprili 1 mabao 2-0, mechi zote mbili zikipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana ‘Black Starlets’ Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Serengeti Boys inatarajiwa kuendelea na mazoezi katika kambi yake ya wiki moja Cameroon, kabla ya Mei 7 kwenda Gabon ambako imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
    Cameroon nayo itashiriki fainali hizo ikiwa imepangwa Kundi A lina timu za wenyeji, Gabon, Guinea na Ghana. Wakati Cameroon watafungua dimba na Ghana Mei 14 Uwanja wa Franceville, Tanzania itaanza na Mali Mei 15 Uwanja wa Port-Gentil, Port-Gentil.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI: SERENGETI BOYS IMEIVA KWA FAINALI ZA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top