• HABARI MPYA

  Thursday, May 11, 2017

  KAGERA SUGAR WADAI SIMBA NDIYO ‘WAMEFOJI’ USAJLI WA MBARAKA YUSSUF ABEID

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Kagera Sugar umesema kwamba, mshambauliji Mbaraka Yussuf Abeid ni mchezaji wao halali na walimsajili baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya Simba.  
  Katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports - Online, Mratibu wa Kagera Sugar, Mohammed Hussein alisema kwamba ni kweli awali walimpokea kwa mkopo mchezaji huyo kutoka Simba SC.
  Hata hivyo, Hussein anasema baadaye mchezaji hiyo aliukana mkataba huo na zikafanyika taratibu za kisheria za kuuvunja kabla ya kusaini mkataba mpya na Kagera Sugar.
  Mbaraka Yussuf Abeid anagombewa na klabu mbili, Kagera Sugar na Simba  “Simba wanatakiwa wawe wawazi na wawafahamishe watu ukweli, kwamba Mbaraka Yussuf Abeid kweli aliletwa kwetu kwa mkopo na kwa barua tu siyo kwa mkataba wowote, kwamba tulipewa barua kwamba yule mchezaji atacheza kwetu kwa mkopo,”alisema.
  Mratibu huyo alisema baada ya kumalizika msimu uliopita, Simba wakamuhitaji Mbaraka Yussuf Abeid arejee, lakini mchezaji mwenyewe akagoma na kusema hakuwahi kusaini mkataba wowote na Wekundu hao wa Msimbazi, hivyo Kagera Sugar wakalifuatilia suala hilo hadi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kujiridhisha kweli hana mkataba na kumpa mkataba.
  Hata hivyo, Hussein alisema kwamba Simba nao wakapeleka jina tofauti na jina halisi la mchezaji huyo kwenye usajili wao wa msimu huu TFF, ili kuudanganya mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na matokeo yake zimetolewa leseni mbili kwa mchezaji mmoja kucheza klabu mbili tofauti msimu mmoja.
  Hivi karibuni, Rais wa Simba SC, Evans Aveva alisema watafungua kesi Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) dhidi ya klabu ya Kagera Sugar, kwa kuwadhulumu mchezaji wao, Mbaraka Yussuf.
  Simba wanadai walimpeleka mchezaji huyo kwa mkopo Kagera Sugar, lakini timu hiyo ikajimilikisha moja kwa moja kinyume cha sharia na bahati mbaya pamoja na kuwasilisha malalamiko TFF, hawajasikilizwa ndiyo maana wanataka kwenda CAS. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERA SUGAR WADAI SIMBA NDIYO ‘WAMEFOJI’ USAJLI WA MBARAKA YUSSUF ABEID Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top