• HABARI MPYA

  Thursday, April 13, 2017

  YANGA YAONDOKA KWA MAFUNGU KUIFUATA MC ALGER

  Na Steven Kinabo, DAR ES SALAAM
  FUNGU la kwanza la wachezaji na viongozi wa Yanga SC limeondoka jioni hii kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, MC Alger Jumamosi.
  Kundi hilo limeondoka majira ya saa 10;00 kwa ndege ya shirika la Emirates Air likiwa na mabeki Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, viungo Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe kupitia Dubai.
  Katika kundi hilo, kulikuwa benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, Msaidizi wake, Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila pia wa Zambia, kocha wa makipa, Juma Pondamali, pamoja na Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.   
  Akizungumza wakati wa safari yao Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, Kocha MsaidizI wa Yanga, Juma MwambusI alisema kwamba kundi la pili litafuatia Saa 2;00 usiku na litaondoka kwa ndege ya shirika la Uturuki likiwa na wachezaji wengine 13 na baadhi ya Maofisa wa timu hiyo likipitia Istanbul.
  Watakaokuwemo kwenye kundi hilo ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Beno Kakolanya; mabeki; Juma Abdul, Oscar Joshua, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Vincent Bossou na Kevin Yondan.
  Viungo ni Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Emmanuel Martin wakati mshambuliaji ni Donald ngoma.  
  Yanga inahitaji sare tu ugenini ili kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili mfululizo mwaka huu, baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mwaka jana, Yanga pia ilicheza hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola ikitoka kutolewa na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAONDOKA KWA MAFUNGU KUIFUATA MC ALGER Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top