• HABARI MPYA

  Sunday, April 16, 2017

  TATIZO KANUNI ZA NCHI HII ZINACHAGUA SEHEMU YA KUFANYA KAZI

  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imeingia doa, baada ya matokeo ya uwanjani ya mchezo namba 194 wa Aprili 2, 2017 kubadilishwa.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, wenyeji Kagera Sugar walishinda 2-1 dhidi ya Simba, lakini wapinzani wao wakapewa pointi tatu na mabao matatu baadaye.
  Hiyo ilifuatia malalamiko ya Simba SC kwa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kwamba Kagera Sugar walimtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi hiyo.
  Kamati ya Saa 72 ilijiridhisha kwamba kweli Fakhi alikuwa ana kadi tatu za njano na kwa mujibu wa kanuni, Simba wakapewa pointi.
  Hakuna tatizo kama kanuni zimefuatwa na Kagera Sugar wanapaswa kuchukua adhabu hiyo ili iwe fundisho siku nyingine wasirudie kosa.
  Miaka kadhaa iliyopita, Simba nao waliwahi kupokonywa pointi pia baada ya ushindi wa uwanjani dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba kwa kosa la kumtumia Mussa Hassan Mgosi Juni 3 mwaka 2006 akiwa ana kadi tatu za njano.
  Hakuna tatizo kama Kagera nao wameingia kwenye mtego wa kukiuka kanuni wakipewa adhabu sawa na waliyopewa Simba mwaka Oktoba 2006.
  Lakini baada ya maamuzi ya Kamati ya Saa 72, kumeibuka hamaki na mijadala inayokinzana.
  Inaonekana kama watu wanapinga Kamati kuipa pointi za mezani Simba, japokuwa inaonekana kanuni inaelekeza hivyo kwa makosa ya aina hiyo.
  Walioumizwa zaidi ni Yanga, mahasimu wa jadi wa Simba na hao ndiyo wanaoongoza mijadala ya hamaki dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Saa 72.
  Yanga imefikia kusema haina imani na Kamati na wametishia kuishitaki Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa madai inashirikiana na viongozi wa Simba kufoji taarifa za kumpakazia Fakhi kadi zaidi.
  Taarifa zote za mechi, ya refa, Kamisaa na Mtathmini huwa haziwekwi wazi – ni mawasiliano ya siri na siku hizi yanatumwa kwa barua pepe, hayapitii posta.
  Maana yake baada ya aliyeiandika, mwingine anayeiona na kuisoma hiyo taarifa ni aliyetumiwa.
  Inapaswa klabu kutunza kumbukumbu zake za kila mechi na Bodi ya Ligi nayo inapaswa kuwa na utaratibu mzuri wa kujua taarifa za wachezaji kila kabla ya mchezo.
  Katika suala hili la Fakhi ni Simba waliowasilisha malalamiko, tena siku tatu baada ya mchezo wao na Kagera wakiwa na vielelezo vyao walivyowasilisha Bodi ya Ligi.
  Watu wanalalamika kwa nini Ligi ya Tanzania hadi leo mshindi anapatikana mezani, wanasahu kwamba dunia nzima bado washindi wanaibuliwa mezani pale tu kanuni zinapokiukwa.
  Mamelodi Sundowns ni mabingwa wa Afrika kwa sasa walitolewa mapema tu hatua ya 32 Bora msimu uliopita kwa mabao ye ugenini baada ya sare ya jumla ya 2-2 na Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakifungwa 1-0 Kinshasa na kushinda 2-1 nyumbani.
  Lakini wakarudishwa kwenye mashindano baada ya kubainika Vita ilimtumia Idrissa Traore akiwa anatumikia adhabu ya kadi nne za njano alizoonyeshwa msimu uliotangulia akiwa anachezea Stade Malien ya kwao, Mali.
  Ni mambo ya kanuni hayo. Lazima yaheshimike na tuwe tayari kuyapokea hata kwa machungu. Hakuna tatizo kabisa hapo.
  Lakini mimi na wewe msomaji wangu tujiulize tatizo liko wapi hadi Yanga ‘mapovu yanawatoka’?.
  Ijumaa ya Desemba 23, mwaka jana mchezaji Venence Ludovic aliichezea African Lyon katika mechi dhidi ya Yanga Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam timu hizo zikitoka sare ya 1-1 wakati akiwa mchezaji halali wa Mbao FC.
  Hata hivyo, Kamati ya Saa 72 ikashindwa kuyatolea uamuzi malalamiko ya Yanga kwa madai mchezaji huyo alipewa leseni kimakosa na Ofisa wa TFF, ambaye hakutajwa jina, ingawa pia ilimzuia mchezaji huyo kuendelea kucheza Ligi Kuu.
  Mwaka 2011 Simba ilirudishwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kutolewa na TP Mazembe ya DRC katika hatua ya 32 Bora kwa jumla ya mabao 6-3 ikifungwa 3-1 Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam.
  Ilirudishwa mashindanoni baada ya kushinda rufaa waliyomkatia beki wa Mazembe wakati huo, Janvier Besala Bokungu ambaye sasa wapo naye.
  Ilibainika Bokungu alikuwa bado mchezaji halali wa klabu ya Esperance ya Tunisia na alivunja mkataba kinyume cha taratibu.
  Simba ikacheza mechi ya mkondo mmoja na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, Misri na kufungwa 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1. 
  Bokungu asingeweza kuichezea Mazembe bila ya leseni ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) – lakini pamoja na hayo, aliiponza klabu ya DRC kutolewa kwenye mashindano.
  Ni kweli Venence Ludovic naye alipewa leseni na TFF aichezee Lyon, lakini kimakosa kama ilivyofanya CAF kwa Bokungu 2011, hivyo hiyo haizuii kanuni kufanya kazi yake.
  Katika hatua za mwanzoni za Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Simba ilimtumia mchezaji Novaty Lufunga akiwa anatumikia adhabu ya kadi za njao, jambo ambalo kikanuni ni kosa ilistahili kuondolewa mashindanoni.
  Inafahamika Ligi Kuu inasimamiwa na Bodi ya Ligi na kamati ya Saa 72, lakini mashindano mengine yapo chini ya Kamati ya Mashindano ya TFF chini ya Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye pia ni Makamu wa Rais wa klabu ya Simba.     
  Hizi za Kombe la TFF maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) ni lawama za Kamati ya Kaburu na si Saa 72 au Bodi.
  Lakini yote yanayofanyika ‘baba wa soka’ ya Tanzania ni TFF chini ya Rais wake, Jamal Malinzi na ndiyo wa kubeba lawama zote.
  Kanuni zilikiukwa Lufunga kutumika kwenye mechi dhidi ya Polisi hatua hazikuchukuliwa. Kanuni zilikiukwa Ludovic kuichezea Lyon dhidi ya Yanga, hatua hazikuchukuliwa.
  Lakini hatua zimechukuliwa baada ya Fakhi kuichezea Kagera Sugar dhidi ya Simba akiwa ana kadi tatu za njano.
  Hapo ndipo tatizo lilipolalia – kwamba kanuni za nchi hii zinachagua sehemu ya kufanya kazi. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TATIZO KANUNI ZA NCHI HII ZINACHAGUA SEHEMU YA KUFANYA KAZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top