• HABARI MPYA

  Sunday, April 09, 2017

  LWANDAMINA SASA ANAANZA KUIPATIA YANGA

  WAKATI fulani gwiji wa soka wa Brazil, Pele aliwahi kuulizwa; Kipi kinamfanya kocha awe bora, akasema; “Awali ya yote –anahitaji kuwa na bahati. Hakuna shaka, -  bahati ni muhimu sana,”.
  Pele alisema hivyo wakati akitoa maoni yake kuhusu klabu ya Manchester United kumchukua kocha Mreno, Jose Mourinho baada ya kuachana na Mholanzi, Louis Van Gaal mwaka jana.
  Akasema; “Kocha  lazima aelewe soka na kuifahamu timu,”.
  Kisha Pele akamwagia sifa zaidi Mourinho, akisema; "Jose Mourinho ni kocha mzuri. Ni kocha mzuri sana sana. Natumaini ana bahati kwa sababu wakati mwingine makocha wazuri hawashindi mashindano,”.
  Kama Pele alikuwa amamsifia Mourinho kwa maslahi yake, lakini mimi nilimuelewa pale aliposema; “Kocha lazima lazima aelewe soka na kuifahamu timu,”.
  Nimeitazama Yanga jana ikicheza na kushinda 1-0 dhidi ya Mouloudia Club Alger ya Algeria katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. 
  Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu nimevutiwa na kiwango cha Yanga na kwa ujumla nidhamu ya uchezaji kama timu na hata mchezaji mmoja mmoja.
  Kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ alikuwa salama sana jana, kutokana na uchezaji mzuri wa safu ya ulinzi kwa ujumla.
  Beki zote za pembeni, Hassan Kessy kulia na Mwinyi Mngwali kushoto zilikuwa zinapanda kusaidia mashambulizi, lakini zilikuwa zinarudi kwa wakati kwenye majukumu yao ya msingi, ulinzi.
  Mabeki wa kati, Mtogo Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ jana walicheza kwa uelewano mkubwa, jambo ambalo lilimfanya Dida awe na kazi nyepesi.
  Sikumbuki wakati gani lango la Yanga lilikuwa kwenye msukosuko wa aina yoyote jana. Safu ya kiungo nayo jana ilicheza vizuri ikiundwa na chipukizi Said Juma ‘Makapu’, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na Mnyarwanda Haruna Niyonzima.
  Kidogo Deus Kaseke aliyekuwa anacheza wingi ya kushoto hakuwa katika ubora wake jana na sikustaajabu alipotolewa kipindi cha pili kumpisha mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma.
  Winga Simon Msuva na kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa walifanya vizuri jana.
  Walilitia misukosuko ya kutosha lango la MC Alger kuanzia kipindi cha kwanza na mapema matumaini ya ushindi kwa Yanga yalianza kuonekana.
  Lakini ni Yanga ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikicheza ovyo na kushinda kwa bahati, mfano mechi na Azam FC wiki iliyopita katika Ligi Kuu.
  Jana Yanga ilishinda 1-0 ikiwa ina uwezo wa kushinda zaidi na mchezo ulimalizika wakati timu hiyo inautawala vizuri tu.
  Wachezaji ni wale wale ambao wamemekuwa wakishindwa kuwafurahisha ipasavyo mashabiki wa Yanga hata jana hawakujitokeza kwa wingi wakihofia matokeo mabaya.
  Na hiyo ni kwa sababu mechi iliyopita ya michuano ya Afrika walilazimishwa sare ya 1-1 na Zanaco nyumbani, hivyo wasiwasi ulikuwa kwa timu ya Algeria labda Yanga ingefungwa.
  Lakini hata kocha ni yule yule, Mzambia George Lwandamina ambaye tayari alikwishaanza kuzungumziwa kufukuzwa kwa sababu timu inasuasua,
  Na kwa ujumla benchi la Ufundi ni lile lile, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Mzambia Noel Mwandila na kocha wa makipa, Juma Pondamali.
  Timu iliyokuwa haichezi vizuri sasa imeanza kucheza vizuri na ukiifuatilia Yanga imekuwa ikiimarika taratibu kutoka ilivyokuwa na sasa inaelekea kurudi katika ubora wake.
  Hapo ndipo nilipokumbuka Pele alichosema kuhusu kocha bora; “Kocha lazima aelewe soka na kuifahamu timu,”.
  Maana yake Lwandamina aliyejiunga na Yanga Novemba, mwaka jana kuchukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm sasa anaanza kuielewa timu kwa sababu hakuna shaka wengi tunajua anaijua soka kwa kuanzia kuicheza enzi zake kama beki hadi timu ya taifa ya nchi yake, Zambia.
  Amekuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia na aliiongoza Zesco United hadi Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa – huwezi kumtilia shaka juu ya uelewa wake kwenye soka, labda akose bahati tu.
  Kitu kimoja naweza kuwaambia wana Yanga Jumapili ya leo, kujenga timu si jambo jepesi – wampe muda Lwandamina, kwa sababu anaijua soka na ndiyo kwanza anaanza kufahamu timu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LWANDAMINA SASA ANAANZA KUIPATIA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top