• HABARI MPYA

  Thursday, September 01, 2016

  TAIFA STARS YAENDA NIGERIA BILA YONDAN, TFF YATAKA TAARIFA YA MKWASA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SENTAHAFU wa Yanga, Kevin Yondani si miongoni mwa wachezaji 18 walioondoka leo Septemba mosi, 2016 kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).
  Taarifa ambazo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imezipata ni kwamba Yondani ana matatizo ya kifamilia ambako hajayaweka sawa hadi timu hiyo inaondoka kwenda Nigeria na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa hajajaza nafasi hiyo.
  Mkwasa amekerwa na kitendo hicho, lakini TFF itasubiri ripoti ya kocha huyo mara baada ya kurejea kutoka Nigeria.
  Kevin Yondan hajaenda na Taifa Stars Nigeria
  Timu hiyo imeondoka na wachezaji 18 huku ikitarajiwa kuungana na na Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta nchini Nigeria. Samatta - Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya Genk ya Ubelgiji anatokea jijini Brussels ambako makocha wake wamemwomba Mkwasa na Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba kumwangalia namna ya kumtumia kwa sababu ya uchovu wa mechi nzito zilizoipa matokeo mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya Uropa Ndogo.
  Taifa Stars inakwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles utakaofanyika Septemba 3, 2016.
  Licha ya mchezo huo kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kwa fainali hizo kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS YAENDA NIGERIA BILA YONDAN, TFF YATAKA TAARIFA YA MKWASA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top