• HABARI MPYA

    Wednesday, September 21, 2016

    SAMATTA NA GENK KATIKA WAKATI MGUMU KIDOGO KAMA MAN UNITED

    Na Mwandishi Wetu, GENK
    KRC Genk Jumapili imefungwa mechi ya tatu mfululizo baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Anderlecht Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.
    Mabao yaliyoizamisha Genk katika mchezo huo ambao Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta hakucheza kabisa yalifungwa na beki Msenegali Serigne Modou Kara Mbodji dakika ya 64 na mshambuliaji Mtunisia, Hamdi Harbaoui dakika ya 76. 
    Genk walipoteza mchezo huo wakitoka kuanza vibaya hatua ya makundi ya Europa League baada ya kufungwa mabao 3-2 na wenyeji Rapid Viena katika mchezo wa Kundi F Alhamisi iliyopita Uwanja wa Allianz, Viena, Austria.
    Na akina Samatta waliingia kwenye mchezo na Rapid Viena wakitoka kufungwa 2-0 na Standard Liege katika Ligi ya Ubelgiji pia. Mara ya mwisho Genk kushinda ilikuwa ni Agosti 28, 2016 waliposhinda 1-0 dhidi ya Zulte-Waregem, bao pekee la kiungo wa Hispania, Alejandro Pozuelo Melero dakika ya 80.
    Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 25 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na saba msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
    Katika mechi hizo, ni 14 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tatu msimu huu, wakati 11 alitokea benchi nane msimu uliopita na tatu msimu huu – na mechi tisa hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na tatu msimu huu.
    Genk watakuwa na mechi mbili mfululizo ugenini, kuanzia leo Uwanja wa Complex Bredestraat mjini Linter dhidi ya Eendracht Aalst Kombe la Ubelgiji na Jumapili dhidi ya Kortrijk Uwanja wa Guldensporen mjini Kortrijk katika Ligi ya Ubelgiji, kabla ya Alhamisi wiki ijayo kurejea kwenye Europa League watakapoikaribisha Sassuolo ya Italia katika mchezo wa pili wa Kundi F.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA NA GENK KATIKA WAKATI MGUMU KIDOGO KAMA MAN UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top