• HABARI MPYA

  Sunday, September 18, 2016

  KILA LA HERI SERENGETI BOYS LEO NA KONGO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuungana pamoja na kuisapoti timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ili iendelee kufanya vizuri.
  Waziri Mkuu aliyasema juzi alipozungumza Bungeni Dodoma, akiipongeza Serengeti Boys kwa matokeo mazuri ya awali na kuitakia kila la heri katika mechi zijazo.
  Serengeti Boys leo inamenyana na Kongo – Brazaville katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Afrika mwakani nchini Madagascar.  Na wataingia uwanjani leo, siku tatu tu tangu warejee nchini kutoka Shelisheli walipoweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na mchezo huo.
  Ikumbukwe Serengeti Boys ilifuzu hatua hii baada ya kuitoa timu ngumu, Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-1 ikishinda 2-0 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza Johannesburg.
  Ni ushindi uliotokana na mabao ya Mohamed Rashid Abdallah kipindi cha kwanza na Muhsin Malima Makame kipindi cha pili katika mchezo ambao Serengeti Boys ililazimika kucheza pungufu tangu dakika ya 44 baada ya kiungo wake wa ulinzi, Ally Hamisi Ng’anzi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.
  Wachezaji wa Serengeti Boys, iliyo chini benchi imara la Ufundi la Serengeti Boys, linaloongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime na Kocha wa makipa na Muharami Mohammed ‘Shilton’ juzi walifanya mazoezi Uwanja wa Taifa na walionekana wako vizuei kuelekea mchezo wa leo.
  Katika kambi yao ya Shelisheli, Serengeti Boys walipata na mchezo mmoja wa kujipima nguvu, ambao walishinda 1-0 dhidi ya Northern Dynamo Uwanja wa Taifa wa Mahe, bao pekee la Muhsin Makame dakika ya 75.
  Serengeti Boys wanahitaji matokeo mazuri leo, ili kutengeneza mazingira mazuri kuelekea mchezo wa marudiano wiki ijayo, ambao ndiyo utaamua timu ya kwenda Madagascar. Kila la heri Serengeti Boys.

  Kilimanjaro Queens wawania fainali Kombe la Challenge leo
  Na Mwandishi Wetu
  TIMU ya taifa ya Tanzania Bara ya wanawake, Kilimanjaro Queens leo inashuka kwenye Uwanja wa Ufundi, Njeru mjini Jinja, Uganda kumenyana na wenyeji, Korongo Jike katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
  Kocha wa Kilimanjaro Queens, Sebastian Nkoma amesema kwamba hakutaka vijana wake kutumia nguvu nyingi katika mchezo wa mwisho wa Kundi B, ili kuzitunza kwa ajili ya Nusu Fainali.
  “Nilijua tutacheza na ama Kenya au Uganda katika Nusu Fainali, zote ni timu ngumu, kwa hiyo tukacheza kwa maarifa sana mechi yetu na Ethiopia, ili tusijichoshe sana na kukwepa pia wachezaji kupata maumivu. Tumefanikiwa na sasa tunaelekeza nguvu zetu katika Nusu Fainali,”alisema Nkoma.  
  Tanzania imeongoza Kundi B baada ya kushinda kura ya sarafu juzi kufuatia sare ya 0-0 na Ethiopia hivyo kufungana nayo kwa pointi na wasatani wa mabao kileleni, wakati Uganda imeshika nafasi ya pili Kundi A nyuma ya Kenya.
  Kwa matokeo hayo, mbali na Kilimanjaro Queens kumenyana na wenyeji Uganda – Nusu Fainali ya itazikutanisha Kenya na Ethiopia.
  Kilimanjaro Queens ilianza vizuri michuano hiyo kwa kuibamiza 3-2 Rwanda, mabao yake yakifungwa na Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika za 11 na 65 na Stumai Abdallah dakika ya 28, wakati ya wapinzani wao yalifungwa na Ibangarrue Marie na Amina Ally wa Tanzania Bara aliyejifunga.
  Fainali ya CECAFA Challenge ya kwanza ya wanawake inatarajiwa kufanyika Septemba 20, ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.
  Samatta katika mtihani mwingine tena Ubelgiji
  Na Mwandishi Wetu
  BAADA ya kuanza vibaya hatua ya makundi ya Europa League baada ya kufungwa mabao 3-2 na wenyeji Rapid Viena katika mchezo wa Kundi F Alhamisi Uwanja wa Allianz, Viena, Austria, mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na timu yake, KRC Genk leo wanarejea kwenye Ligi ya Ubelgiji.
  Samatta na Genk yake leo watakuwa wenyeji wa Anderlecht Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, wakitoka kufungwa mechi mbili mfululizo, ukiwemo wa Jumapili iliyopita walipofungwa 2-0 na Standard Liege katika Ligi ya Ubelgiji pia.
  Samatta amecheza mechi mbili mfululizo bila kufunga bao, kwani Alhamisi mabao ya Genk yalifungwa na Leon Bailey yote, la kwanza dakika ya 29 na la pili dakika ya 90 kwa penalty, huku ya wenyeji, Rapid Viena yakifungwa na Stefan Schwab dakika ya 51, Joelinton Cassio Apolinario de Lira maarufu tu kama Joelinton dakika ya 59 na Omar Colley aliyejifunga dakika ya 60.
  Mchezo mwingine wa kundi hilo, wenyeji Sassuolo walishinda 3-0 dhidi ya Athletic Athletic Bilbao ya Hispania Uwanja wa Citta del Tricolore, mabao ya Pol Lirola dakika ya 60, Gregoire Defrel dakika ya 75 na Matteo Politano dakika ya 82.
  Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 25 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na saba msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
  Katika mechi hizo, ni 14 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tatu msimu huu, wakati 11 alitokea benchi nane msimu uliopita na tatu msimu huu – na mechi tisa hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na tatu msimu huu.

  Ngassa mezani na Rais wa Fanja leo Oman
  Na Mwandishi Wetu
  KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa leo anatarajiwa kuwa na kikao na Mwenyekiti wa klabu ya Fanja ya Oman, Sheikh Saif Abdullah Al-Sumri.
  Ngassa alitua Oman Alhamisi kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho ambayo kama yatakwenda vizuri, atajiunga na timu hiyo inayocheza Ligi ya Mabingwa ya Asia.
  Na mchezaji hu o wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC, Azam FC na Simba za Dar es Salaam anakwenda y Oman, kiasi cha wiki mbili tangu avunje mkataba na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
  "Unajua huku kuanzia Ijumaa ndiyo mapumziko, watu hawafanyi kazi. Sasa mimi nilifika Alhamisi, ila Jumapili ndiyo nitakuwa na mazungumzo na Rais wa Fanja,”alisema Ngassa akizungumza na Lete Raha juzi usiku kutoka Muscat, Oman.
  Ngassa alijiunga na Free State Stars Mei mwaka jana akisajiliwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne.
  Hata hivyo, kocha aliyemsajili baba huyo wa Farida (9) na Faria (7) alifukuzwa baada ya miezi miwili tu na sasa tayari yuko Mbeya City ya Tanzania.
  Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuwa Free State, Ngassa alifanya kazi na makocha wanne akiwemo huyu wa sasa, Mfaransa Denis Lavagne aliyeanza kazi Juni mwaka huu.
  Wengine ni Mjerumani Ernst Middendorp aliyefanya kazi kati ya Septemba na Desemba 2015, Mtaliano Giovanni Solinas aliyefanya kazi kati ya Desemba na Mei 2016.
  Na Lavagne ndiye aliyechangia Ngassa kuomba kuondoka Free State baada ya kuonyesha kuidharau Tanzania haiwezi kuwa na mchezaji bora.
  Lavagne alimuanzishia benchi Ngassa katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya ABSA ya Afrika Kusini Agosti 23, kabla ya kumuingiza dakika ya 63 kwenda kuchukua nafasi ya Mbuyiselo Thethani wakati huo tayari FS imekwishapigwa 2-1, matokeo yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo.
  Na baada ya kuingia Ngassa akaenda kucheza kwa kiwango kizuri na kukaribia kufunga mara mbili hadi kocha huyo akampongeza baada ya mchezo, ingawa tayari mchezaji wa Tanzania alikwishatumbukiwa nyongo na Mfaransa huyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI SERENGETI BOYS LEO NA KONGO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top