• HABARI MPYA

    Tuesday, August 02, 2016

    WIKI TATU TU ZA MAKOCHA KUTOKA HISPANIA, AZAM IMEBADILIKA KWA MENGI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, ilirejea jana jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza kambi ya wiki moja visiwani Zanzibar, ambayo ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao.
    Ikiwa visiwani humo, Azam FC mbali na kujifua vilivyo pia ilipata fursa ya kucheza mechi mbili za kirafiki, wa kwanza ikicheza na Kombaini ya Wilaya Mjini na wa pili walikipiga na Taifa ya Jang’ombe, zote ilishinda bao 1-0.
    Unaweza kujiuliza ni kwanini ushindi kiduchu hivyo, kiukweli licha ya washambuliaji kukosa nafasi nyingi za wazi lakini Kocha Mkuu Zeben Hernandez, kwa sasa yupo kwenye kazi kubwa ya kukisuka kikosi kuingia kwenye mfumo wake.
    Kwa mujibu wa maelezo yake, jambo kubwa analolizingatia hivi sasa ni kusuka eneo lake la ulinzi pamoja na kuifanya timu yake kwa nafasi kupitia mfumo wake na kwa sasa mabao yanakuja kama ziada tu, lakini hayo hayajamnyima nafasi ya kusema kuwa ana tatizo kubwa la ufungaji wa mabao ndani ya kikosi chake.
    Wakati kikosi cha Azam FC kikiwa mapumzikoni leo Jumatatu kikitarajia kurejea mazoezini kesho Jumanne asubuhi. Mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz unakuletea manufaa ya kambi ya timu hiyo Zanzibar pamoja na wiki tatu za makocha kutoka Hispania tokea walipoanza kuifundisha timu hiyo.

    Matayarisho ya kisasa
    Azam FC ikiwa Zanzibar ilivutia watu wengi na hii ni kutokana na programu za matayarisho iliyokuwa ikitolewa na makocha wa kikosi hicho.
    Kocha Mkuu Zeben na Msaidizi wake,Yeray Romero, Kocha Msaidizi wa Viungo, Pablo Borges, wa Makipa Jose Garcia na Daktari Sergio Perez Soto, waliwateka watu kutokana na kufanya programu tofauti tofauti za mazoezi kila siku.
    Makocha hao hawakuishia programu za uwanjani tu bali hata zile za nje ya uwanja, ambazo baadhi yao ni zile za kufanya mazoezi makali ufukweni, kufanya mazoezi ndani ya bwawa la kuogelea (swimming pool) pamoja na ile mpya kabisa ya wachezaji kuendesha baiskeli barabarani, ambayo hufanywa hata na timu kubwa barani Ulaya.
    Mpaka sasa makocha hao wakiwa wamefikisha wiki tatu za mazoezi yao wakiwa na lengo kubwa la kuifanya Azam FC kuwa timu ya kisasa ndani na nje ya uwanja, tayari mwanga huo umeshaanza kuonekana kwa wachezaji kutokana na programu za kisasa wanazopewa zinazoendana na vifaa vya kisasa vya ufundishaji.

    Mfumo wa uchezaji
    Kama inavyojulikana ujio wa makocha hao kutoka Hispania ni kuifanya Azam FC icheze soka la kuvutia pamoja na mafanikio Kitaifa na Kimataifa, kwa muda mchache tu waliopo mpaka sasa timu imeonekana kubadilika kwenye mfumo wa kiuchezaji.
    Azam FC kwa siku za hivi karibuni kwenye mechi zake za majaribio, imekuwa ikionekana kucheza soka la kueleweka tokea inapoanzisha mpira hadi kufika kwenye eneo la hatari la timu pinzani huku wachezaji wakicheza kwa nidhamu kubwa.
    Lakini tatizo kubwa linalowakabili wachezaji wa Azam FC ni ugeni wa mifumo mipya wanayopewa na makocha hao, jambo ambalo tayari Zeben amelitolea ufafanuzi akisema itawachukua mwaka mzima wachezaji kuweza kuushika ipasavyo mfumo wake wote.
    Hivyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo tunaweza kuishuhudia Azam FC mpya kabisa itakayokuwa ikitisha zaidi kila idara, ikijitambulisha yenyewe kupitia soka safi inalocheza na litakaloipatia matokeo bora uwanjani.

    Ukabaji wa hali ya juu
    Timu bora iliyokamilika haiangaliwi tu namna inayokuwa ikimiliki mpira bali jicho jingine hutupiwa pale inapokuwa haina mpira, Je, inawezaje kuurejesha mpira kwenye himaya yao pale inapopokonywa na mpinzani?
    Azam FC katika mechi zake za majaribio ilizocheza awali Azam Complex na ikiwa kambini Zanzibar, imekuwa na uwezo mkubwa sana wa ukabaji pale inapokuwa haina mpira, hii ikiwa ni sehemu ya mafundisho ya Zeben ambayo amekuwa akiyafanyia kazi mara kwa mara mazoezini.
    Mabingwa hao wanaodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi kabisa cha Azam Cola, wachezaji wake wamekuwa na pumzi ya kutosha kwenye mechi wanazocheza, huku wakianza kukaba kwa pamoja kutoka eneo la ushambuliaji hadi ulinzi jambo ambalo limekuwa likiwapa shida sana timu pinzani ilizocheza nazo mpaka sasa.

    Inatisha kwa ufiti
    Programu ya mazoezi makali ya viungo wanayoendelea kupewa wachezaji, imefanikiwa kuwasaidia sana wachezaji mpaka sasa wakiwa wanaonekana na nguvu kubwa.
    Hata pale wanapogombea mpira na wachezaji wa timu pinzani nguvu hiyo imekuwa ikionekana kwa wachezaji wa Azam FC kushinda mipira kirahisi huku wakionekana wanafanya sana rafu kumbe hiyo inatokana na ufiti waliokuwa nao.
    Hivi sasa kila mchezaji amepewa programu yake ya mazoezi ya ‘gym’ kulingana na mwili wake ulivyo, ambayo hutakiwa kufanya kila siku kabla ya mazoezi ya pamoja asubuhi.

    Kubadilishwa namba
    Moja ya vitu ambavyo bado makocha wa Azam FC wanavifanyia kazi ni kuwajaribu wachezaji waliokuwa nao kikosini kucheza namba tofauti tofauti uwanjani.
    Wachezaji ambao mpaka sasa wameweza kuchezeshwa namna tofauti ni Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, ambaye alitolewa kwenye eneo la kiungo wa ukabaji alilolizoea hadi beki wa kati akicheza na Aggrey Morris.
    Baada ya Zeben kumaliza kumjaribu Himid katika nafasi hiyo, kwenye kambi ya visiwani Zanzibar alihamia kwa kiungo mkabaji Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, ambaye katika mechi zote mbili za huko alimchezesha beki ya kati sambamba na Aggrey.
    Migi aliyewahi kucheza nafasi hiyo kwenye mechi ya African Lyon msimu uliopita, ameonekana kufanya vizuri sana katika kutekeleza majukumu ya namba hiyo jambo ambalo limewafurahisha makocha.
    Wachezaji wengine waliobadilishwa namba ni mabeki wa kati David Mwantika na kinda Ismail Gambo, ambao kwa sasa wanachezeshwa kama mabeki wa upande wa kulia.  

    Umakini kwenye usajili
    Timu bora siku zote hujengwa na muunganiko wa wachezaji bora ili kufikia mafanikio yaliyokusudiwa, wakati Azam FC ikiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya makocha wa timu hiyo wamefanikiwa kuwa makini kwenye usajili.
    Mpaka sasa zoezi la usajili likiwa linaendelea, wachezaji kadhaa wamepata nafasi ya kufanya majaribio ya kujiunga na Azam FC, lakini imekuwa ni ngumu kwa makocha hao kufanya uamuzi wa haraka wa kusema mchezaji fulani asajiliwe.
    Wachezaji ambao mpaka sasa wamemaliza wiki mbili na bado wanaendelea kujaribiwa ni Fuadi Ndayisenga, Ibrahima Fofana, Bruce Kangwa huku Brian Abbas akiwa ametimiza siku ya sita sasa tokea aanze majaribio.
    Azam FC mpaka sasa imeshakamilisha usajili wa winga kutoka Medeama ya Ghana, Enock Atta Agyei (18), ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili wiki iliyopita na ameshatua nchini tokea Jumamosi iliyopita tayari kabisa kuanza mazoezi.

    Kila kitu umoja
    Namna pekee ya timu yoyote kufikia mafanikio yaliyokusudiwa si tu kuishia kwenye kusajili wachezaji bora na kuchukua makocha bora, bali suala la kutengezeza mshikamano na umoja ndani ya timu nalo ni moja ya jambo kubwa sana la kufanikisha hilo.
    Ukiingalia Azam FC hivi sasa imebadilika sana hasa linapokuja suala la umoja, makocha wapya wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha umoja ndani ya timu, ambapo kila kitu wachezaji hufanya kwa umoja bila kutengana.
    Ni jambo la kufurahisha sasa hivi ukiona namna wachezaji wa Azam FC wanaposhangilia mabao yao kwenye mechi hizi za majaribio, kwani wamekuwa wakipongezana kwa pamoja wakia na furaha ya pamoja kila wanapofunga.

    Hakuna masikhara
    Moja ya mambo makubwa ambayo makocha wapya wamefanikiwa kudhibiti, ni kujenga nidhamu kubwa kwa wachezaji ndani na nje ya uwanja.
    Makocha hao wamekuwa wakisisitiza nidhamu kwa wachezaji pale linapokuja suala la kazi iliyowafanya wawe Azam FC na hakuna muda wa masikhara, na ili kulidhibiti suala hilo wamefanikiwa kuweka sheria mbalimbali kwa wale watakaoshindwa kwenda kinyume na hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WIKI TATU TU ZA MAKOCHA KUTOKA HISPANIA, AZAM IMEBADILIKA KWA MENGI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top