• HABARI MPYA

  Wednesday, April 20, 2016

  YANGA KAZI MOJA TU LEO ALEXANDRIA, AL AHLY WAKOME!

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MACHO na masikio ya Watanzania wengi leo yanaelekezwa mjini Alexandria, Misri ambako Yanga SC itakuwa ikimenyana na wapinzani wao wa kihistoria kwenye michuaano ya Afrika, Al Ahly.
  Mchezo huo wa marudiano hatua ya 16 Bora unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa jeshi wa Borg El Arab kuanzia Saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
  Na katika mchezo huo, Yanga inatakiwa kushinda ugenini au kutoa sare ya mabao kuanzia 2-2 ili kusonga mbele baada ya awali kulazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga iliyofikia katika hoteli Panacea mjini humo, jana usiku ilifanya mazoezi yake ya mwisho Uwanja wa Borg El Arab na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm mwishoni aliwafanyisha mtihani wa kupiga penalti wachezaji wake – kwa sababu ikitokea mchezo huo ukaisha kwa sare ya 1-1 matuta yataamua mshindi.
  Kikosi cha Yanga kilichotoa sare ya 1-1 na Al Ahly mjini Dar es Salaam

  Mshindi wa jumla wa mchezo huo ataingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati atakayetolewa ataangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. 
  Hii inakuwa mara ya tano, Yanga kukutana na Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mara zote nne za awali timu ya Jangwani, Dar es Salaam ikitolewa. 
  Mara ya kwanza wababe hao walikutana mwaka 1982 katika Raundi ya Pili na Yanga ikatolewa kwa jumla ya 6-1 ikifungwa 5-0 Cairo na kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Mwaka 1988 zikakutana katika Raundi ya Kwanza na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 4-0 waliyofungwa Cairo baada ya kutoka sare ya 0-0 Dar es Salaam.
  Mwaka 2009 Yanga wakatolewa kwa jumla ya mabao 4-0 wakifungwa 3-0 Cairo na 1-0 Dar es Salaam katika Raundi ya Kwanza pia.
  Yanga ikaandika historia mwaka 2014 ilipowafunga kwa mara ya kwanza Al Ahly Dar es Salaam 1-0, bao pekee la Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kabla ya kwenda kufungwa 1-0 mjini Alexandria. Mchezo ukarefushwa hadi dakika 120 kabla ya Ahly kushinda kwa penalti 4-3.
  Kwa ujumla, Yanga haijawahi kuitoa timu yoyote ya Kaskazini mwa Afrika kwenye michuano ya Afrika na Al Ahly inakuwa timu pekee ya huko kuwahi kufungwa na mabingwa hao wa Tanzania.
  Mwaka 1992, Yanga ilitolewa na Ismailia ya Misri katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa, ikifungwa 2-0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kulazimisha sare ya 1-1 Cairo.
  Mwaka 1998 Yanga ilifungwa 6-0 na Raja Casablanca ya Morocco katika mchezo wa Kundi B Ligi ya Mabingwa kabla ya kutoa sare ya 3-3 mchezo wa marudiano Dar es Salaam.
  Mwaka 2000 Yanga ililazimishwa sare ya 1-1 na Zamalek ya Misri mjini Dar es Salaam katika iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi kabla ya kwenda kufungwa 4-0 Cairo katika Raundi ya Kwanza.
  Mwaka 2007 Yanga ilifungwa 3-0 na Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutoa sare 0-0 Mwanza.
  Yanga iliingia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kutolewa na El Merreikh ya Sudan, ikitoa sare ya 0-0 Mwanza na kufungwa 2-0 Khartoum.
  Mwaka 2008 Yanga ilifungwa 1-0 na Al Akhdar ya Libya mjini Tripoli kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam katika Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika. 
  Mwaka 2012 Yanga ililazimisha sare ya 1-1 na Zamalek ya Misri mjini Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 1-0 mjini Cairo.
  Zote zinafundishwa na makocha Waholanzi, Yanga ikiwa na Hans van der Pluijm mwenye umri wa miaka 67 na Ahly ikiwa na Maarten Cornelis Jol maarufu kama Martin Jol, mwenye umri wa miaka 60.
  Vikosi vya leo vinatarajiwa kuwa; Al Ahly; Sherif Ekramy, Mohamed Hany, Sabry Raheel, Rami Rabea, Ahmed Hegazy, Ahmed Fathi, Abdallah Said, Hossam Ghally, Amri Gamal, Ramadan Sobhi na Malick Evouma.
  Yanga; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Simon Msuva.
  Je, Yanga itaweza kuvunja mwiko wa kutolewa na Al Ahly na kwa ujumla timu za Kaskazini mwa Afrika michuano ya CAF? Bila shaka inawezekana. Kila la heri Yanga. Mungu ibariki Yanga. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KAZI MOJA TU LEO ALEXANDRIA, AL AHLY WAKOME! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top