• HABARI MPYA

    Tuesday, April 05, 2016

    JUMA ABDUL YUKO FITI KUIVAA AL AHLY JUMAMOSI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAAM
    BEKI tegemeo wa kulia wa Yanga, Juma Abdul Jaffar Mnyamani anatarajiwa kuanza mazoezi leo, baada ya kupata nafuu ya maumivu ya misuli.
    Juma Abdul alitolewa kwa machela juzi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar na nafasi yake kuchukuliwa na beki wa kati, Pato Ngonyani dakika ya 90 na ushei baada ya kuumia misuli.
    Na hiyo ilizua hofu kwa mashabiki wa Yanga kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.
    Hata hivyo, baada ya matibabu mazuri kuanzia juzi usiku, beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar ya Morogoro na Toto Africans ya Mwanza sasa yuko fiti.
    Juma Abdul yuko fiti kucheza dhidi ya Al Ahly Jumamosi Uwanja wa Taifa 

    “Najisikia vizuri kwa sasa, nilishitua misuli kidogo tu, natarajia kuanza mazoezi kesho (leo),”alisema jana beki huyo mwenye mashuti makali.
    Yanga SC imeingia kambini kisiwani Pemba kujiandaa na mchezo dhidi ya wapinzani wao wa kihistoria kwenye michuano ya Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana Aprili 19 mjini Cairo, Misri.
    Wachezaji wote wa Yanga akiwemo Haruna Niyonzima ambaye anasumbuliwa na Malaria na pia hatacheza mechi ya kwanza dhidi ya Al Ahly kutokana na kuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano wapo Pemba na leo wanaanza mazoezi Uwanja wa Gombani.
    Kikosi cha Yanga kilichoingia kambini jana ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.
    Mabeki ni Juma Abdul, Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Pato Ngonyani, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Viungo ni Salum Telela, Mbuyu Twite (DRC), Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Deus Kaseke, Godfrey Mwashiuya na Issoufou Boubacar (Niger).
    Washambuliaji ni Paul Nonga, Matheo Anthony, Malimi Busungu, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe). 
    Benchi la Ufundi ni Kocha Mkuu, Hans van der Pluijm (Uholanzi), Kocha Msaidizi, Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali
    Daktari, Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa, Mohammed Mpogolo na Meneja, Hafidh Saleh. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUMA ABDUL YUKO FITI KUIVAA AL AHLY JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top