• HABARI MPYA

  Monday, March 07, 2016

  YANGA KUONDOKA ALHAMISI KUWAFUATA APR LIGI YA MABINGWA AFRIKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC watapiga mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya African Sports Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumanne ya kesho na mapema Alhamisi watapanda ndege kwenda Rwanda kuifuata APR.
  Yanga watakuwa wageni wa APR katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi Uwanja wa Amahoro, Kigali nchini Rwanda, kabla ya timu hizo kurudiana wiki moja baadaye Dar es Salaam.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba kikosi cha timu yao hakijavunja kambi baada ya mechi na Azam FC mwishoni mwa wiki.
  Yanga watacheza na African Sports kesho kabla ya Alhamisi kwenda Kigali

  Yanga ililazimishwa sare ya 2-2 na Azam FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Ligi Kuu, na baada ya mechi hiyo wachezaji walirejea kambini kujiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya African Sports.
  “Baada tu ya mchezo wetu na Sports, Alhamisi tutapanda ndege kwenda Kigali, maandalizi ya safari yamekamilika,”amesema Muro.
  Kwa ujumla, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itaendelea katikati ya wiki na mbali na kesho mabingwa hao watetezi, Yanga SC kuwakaribisha African Sports keshokutwa kutakuwa na mechi nyingine.
  Prisons itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Coastal Union na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Mwadui FC na Majimaji Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, JKT Ruvu na Toto Africans Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani – wakati Alhamisi Simba SC wataikaribisha Ndanda FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Mbeya City watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Sokoine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUONDOKA ALHAMISI KUWAFUATA APR LIGI YA MABINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top