• HABARI MPYA

  Saturday, March 05, 2016

  NI ‘MSHIKE MSHIKE’ YANGA NA AZAM TAIFA LEO, SI YA KUSIMULIWA

  REKODI YA YANGA NA AZM FC: 
                      P W D L GF GA GD Pts
  Yanga SC 19 7 5 7 24 23 1 26
  Azam FC 19 7 5 7 23 24 -1 26
  Winga wa Azam FC, Farid Mussa akiwatoka mabeki wa Yanga, Juma Abdul na Nadir Haroub 'Cannavaro' Oktoba 17, mwaka jana

  MECHI ZILIZOPITA ZA AZAM NA YANGA:
  Oktoba 17, 2015 
  Yanga SC 1-1 Azam (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Agosti 22, 2015
  Yanga 0-0 Azam FC (Yanga ilishinda kwa penalti 8-7 Ngao ya Jamii)
  Julai 29, 2015
  Azam 0-0 Yanga SC (Azam ilishinda kwa penalti 5-3 Robo Fainali Kombe la Kagame)
  Mei 6, 2015
  Azam 2-1 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Desemba 28, 2014
  Yanga SC 2-2 Azam (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Septemba 14, 2014
  Yanga SC 3-0 Azam FC (Ngao ya Jamii)
  Machi 19, 2014; 
  Yanga SC 1-1 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Septemba 22, 2013; 
  Azam FC 3-2 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Februari 23, 2013;  
  Yanga SC 1-0 Azam FC (Ngao ya Jamii)
  Novemba 4, 2012;  
  Azam FC 0-2 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Machi 10, 2012; 
  Yanga SC 1-3 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  January 07, 2012
  Azam FC 3-0 Yanga SC (Robo Fainali Kombe la Mapinduzi)
  Septemba 18, 2011;  
  Azam 1-0 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Machi 30, 2011;  
  Yanga SC 2-1 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Oktoba 24, 2010; 
  Azam FC 0-0 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Machi 7, 2010;  
  Yanga SC 2-1 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Oktoba 17, 2009; 
  Azam FC 1-1 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Aprili 8, 2009;  
  Yanga SC 2-3 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  Oktoba 15, 2008;  
  Azam FC 1-3 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
  (Rekodi hii inahusisha mechi za mashindano tu, tangu Azam na Yanga wanaanza kukutana)
  Nahodha wa Azam FC akiurukia mpira wa juu dhidi ya beki wa Yanga, Kevin Yondan


  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWELEKEO wa wapi taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara litaelekea msimu huu tutaanza kuuona leo baada ya mchezo baina ya timu mbili zinazoongoza mbio za taji hilo.
  Yanga, mabingwa watetezi wanatarajiwa kumenyana na Azam FC kuanzia Saa 10:00 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo ambao mshindi atapanda kileleni na kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi tatu. Zote zina pointi 46, kila moja baada ya kucheza mechi 19, ingawa Yanga wapo kileleni kwa wastani wa mabao. 
  Ni pambano la pili kuzikutanisha timu hizo mwaka huu, na la tano kwa ujumla msimu huu tangu zilipokutana katika Kombe la Kagame Julai mwaka jana, kila timu ikishinda mara moja na nyingine zote kutoka sare.
  Julai 29, mwaka jana, timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake iliifunga Yanga SC kwa penalti 5-3 katika Robo Fainali ya Kombe la Kagame kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
  Agosti 22, mwaka huu, Yanga SC ikalipa kisasi baada ya kushinda kwa penalti 8-7 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika mchezo wa Ngao ya Jamii kabla ya sare mbili mfululizo za 1-1, kwanza kwenye Ligi Kuu Oktoba 17, mwaka jana na baadaye kwenye Kombe la Mapinduzi Januari 5, mwaka huu.
  Viungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima (kuiia) na Jean Baptiste Mugiraneza wa Azam (kushoto) wanaweza kukutana tena uwanjani leo

  Oktoba 17, mwaka jana Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 45 kupitia kwa Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma aliyepokea krosi ya Juma Abdul na kuwachambua mabeki wa Azam kisha kupachika mpira nyavuni – kabla ya Muivory Coast Kipre Tchetche aliyetokea benchi kipindi cha pili kwenda kuchukua nafasi ya Mkenya Allan Wanga kuifungia Azam bao la kusawazisha dakika ya 83 akimalizia pasi ya Farid Mussa.
  Katika mchezo huo, Yanga walipata penati baada ya kipa wa Azam Aishi Manula kumuangusha winga wa Yanga Simon Msuva kwenye eneo la hatari, lakini kiungo Mzimbabwe Thabani Kamusoko akampelekea mikononi kipa wa Azam shuti lake.
  Na Januari 5, licha ya Azam FC kucheza pungufu baada ya Azam FC kumpoteza Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyeonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Mfaume Ali Nassor dakika ya 62, lakini ikamudu kumaliza mechi kwa sare ya 1-1.
  Azam FC walitangulia kupata bao dakika ya 58 baada ya shambulizi la kushitukiza – sifa zimuendee mfungaji wa bao hilo, Kipre Herman Tchetche raia wa Ivory Coast aliyewakokota mabeki watatu wa Yanga SC hadi karibu kabisa na boksi na kufumua shuti lililompita kipa Deo Munishi ‘Dida’. 
  Lakini beki Mtogo, Vincent Bossou aliisawazishia Yanga SC dakika ya 83 akimalizia mpira ulioparazwa kwa kichwa na Malimi Busungu baada ya kona ya Simon Msuva.
  Na kwa ujumla mchezo wa leo ni 19 wa mashindano kuzikutanisha timu hizo, ikiwemo Ligi Kuu, Kombe la Kagame na Kombe la Mapinduzi, kila timu ikishinda mechi saba, moja kati ya hizo kila timu imeshinda kwa penalti, zimetoka sare mara tano na Yanga imefunga mabao 24, wakati Azam imefunga mabao 23. 
  Makocha wa timu zote, Stewart John Hall raia wa Uingereza anayefundisha Azam FC na Mholanzi Hans vad der Pluijm wa Yanga wanajua mchezo wa leo utakuwa mgumu.
  Mara ya mwisho zilipokutana katika Kombe la Mapinduzi, Uwanja wa Amaan, Zanzibar mapema mwaka huu mechi ilitawaliwa na undava na Nahodha wa Azam, John Bocco aliondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu timu hizo zikitoka 1-1.
  Hall alimvaa Pluijm baada ya kipindi cha kwanza akataka kumchapa makofi, lakini baadaye akajutia uamuzi wake na kabla ya kuanza kipindi cha pili wakamaliza tofauti zao.
  Yanga wanaingia uwanjani wakitokea kwenye kambi ya wiki moja kisiwani Pemba, wakati FC wanatokea makao makuu yao, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Ni mechi ya mshike mshike mzito Yanga na Azam, wakati mwingine inafikia hata viongozi kununiana na mashabiki kuchapana makonde. Leo Taifa kazi ipo!
  Beki Serge Wawa wa Azam FC , raia wa Ivory Coast (kushoto) na mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga SC, DOnald Ngoma wanatarajiwa kuwa burudani ya ziada leo Uwanja wa Taifa
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI ‘MSHIKE MSHIKE’ YANGA NA AZAM TAIFA LEO, SI YA KUSIMULIWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top