• HABARI MPYA

    Monday, March 14, 2016

    KOCHA AZAM FC ASEMA MORRIS AMERUDI KAMILI KUONGEZA NGUVU VITA YA UBINGWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica raia wa Romania amesema beki wa kati Aggrey Morris sasa yuko fiti kwa asilimia 100 kuisaidia klabu hiyo katika kampeni za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Urejeo wa Aggrey Morris?
    Aggrey Morris alirejea uwanjani Jumamosi kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje tangu Oktoba mwaka jana kutokana na maumivu ya goti na akaiongoza timu kushinda 3-0 ugenini katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
    "Ametoka kwenye majeraha makubwa na ameonyesha kiwango kizuri leo (Jumamosi) ni ngumu kusema alikuwa mchezaji bora uwanjani, lakini ni mmoja wa wachezaji waliowadhibiti wachezaji wa Bidvest na sisi kutofungwa bao ugenini,” alisema Mario.
    Aggrey Morris (kushoto) akifurahia na Himid Mao (katikati) na Erasto Nyoni (kulia) baada ya mechi na Bidvest
    Kocha Mkuu, Stewart Hall akimpa 'tano' Aggrey Morris baada ya mechi hiyo



    Aidha, Mromania huyo amesema kuwa hawatabweteka na matokeo mazuri ya awali waliyopata ugenini dhidi ya Bidvest Wits badala yake watapambana hadi dakika ya mwisho kuelekea mchezo wa marudiano Jumapili ijayo (Machi 20).
    Azam FC inayodhaminina na Benki ya NMB ambayo ni bora kabisa nchini Tanzania, ilirejea nchini jana na moja kwa moja kuingia kambini, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Kabla ya mchezo huo wa marudiano, Azam FC keshokutwa Jumatano itashuka tena dimbani kuvaana na Stand United katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex.
    Na Marinica amesema kuwa wanatakiwa kuwa waangalifu na kujua mbinu watakazokuja nazo wapinzani wao na namna watakavyouchulia mchezo huo wa marudiano.
    Alisema tokea mwanzoni mwa mwaka huu waliposhiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, walijua ya kuwa wanaenda kucheza na Bidvest Wits, hivyo hadi wanafanikiwa kudhibiti mbinu zao wamefanikiwa kuwasoma kwenye mechi takribani sita, tano kupitia DVD na moja wakiwaangalia ‘live’ nchini Seychelles walipocheza na Light Stars.
    “Hatuwezi kuanza kufikiria kuwa tayari tumeshavuka kufuatia ushindi huo, kwenye mpira huwezi kusonga mbele kabla ya dakika ya mwisho ya mchezo wa mwisho, hivyo pia tunatakiwa kujua ni wachezaji gani watakaopatikana baada ya mchezo wa Jumatano (Stand United) tunaye mtaalamu wa viungo ambaye atatuambia yupi mchezaji ana matatizo ambaye hatakuwepo kwenye mchezo huo wa marudiano,” alisema.
    Akizungumzia mchezo huo wa kwanza, Mario alisema wachezaji wote walifanikiwa kuonyesha viwango vizuri uwanjani kwa kupambana na kucheza kupitia mbinu walizowafundisha kukabiliana na wapinzani wao huku akidai kuwa Azam FC ni timu bora kabisa na walifanikiwa kuonyesha ubora wao kwenye mchezo huo.
    “Ni ngumu kusema sehemu gani ilicheza vizuri, kitu ninachoweza kusema kila sehemu ilifanikiwa kucheza vizuri kuanzia kwa Aishi (Manula) langoni, sehemu ya ulinzi, kiungo na hata eneo la ushambuliaji, kilikuwa ni kiwango kizuri usiku huo kwa kweli kwa timu yetu.
    “Kikubwa sisi kama benchi la ufundi tuliweza kujua ubora wao wa kutumia mipira ya adhabu ndogo na krosi na hatukuwapa mwanya huo, tulicheza kwa staili yetu na tulimiliki mpira na kuwanyima mpira wao hii iliwapa wakati mgumu kwenye mchezo huo na kweli mbinu yetu ilifanikiwa,” alisema.
    Kuelekea mchezo dhidi ya Stand United, alisema kuwa jambo la kwanza wataangalia wachezaji waliofiti kuelekea mchezo huo huku akitanabaisha kuwa lengo lao ni kupata ushindi katika mchezo huo ili kuendeleza mbio za kuwani ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA AZAM FC ASEMA MORRIS AMERUDI KAMILI KUONGEZA NGUVU VITA YA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top