• HABARI MPYA

  Monday, March 14, 2016

  LIGI KUU BARA YAZIDI KUNOGA, SPORTS NA MBEYA CITY KUKINUKISHA MKWAKWANI LEO, AZAM FC WANA STAND UNITED CHAMAZI JUMATANO

  RATIBA LIGI KUU YA VODACOPM TZ BARA
  Machi 14, 2016
  African Sports Vs Mbeya City
  Machi 16, 2016
  Azam FC Vs Stand United
  Machi 18, 2016
  Kagera Sugar Vs Mtibwa Sugar
  Machi 19, 2016
  Coastal Union Vs Simba SC
  Azam FC Vs JKT Ruvu
  Majimaji Vs Mbeya City
  Stand United Vs Ndanda FC
  Machi 20, 2016
  African Sports Vs Prisons
  Machi 21, 2016
  Mgambo JKT Vs Toto Africans
  Machi 22, 2016
  Mtibwa Sugar Vs Azam FC
  Machi 23, 2016
  Yanga SC Vs Mwadui FC
  Machi 24, 2016
  African Sports Vs Toto Africans
  African Sports wapo mguu mmoja Ligi Kuu na leo wapo vitani kuepuka kushuka daraja

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja tu, African Sports wakiikaribisha Mbeya City Uwanja wa Mkwakwani, Tanga katika vita ya kuepuka kushuka daraja.
  African Sports inashika mkia katika Ligi Kuu ya timu 16, baada ya kuambulia pointi 17 tu katika mechi 22 ilizocheza hadi sasa, wakati Mbeya City ni ya tisa ikiwa na pointi 24 za mechi 22, ambazo bado haziwahakikishii kubaki Ligi Kuu.
  Maana yake, Mbeya City inayofundishwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri itahitaji ushindi leo ili kuendelea kujiondoa kwenye maeneo ya hatari.
  African Sports ya kocha Aluko Ramadhani wazi ikiwa katika msimu wake wa kwanza tangu ipande Ligi Kuu – inapambana kutafuta nafasi ya kubaki kwenye michuano hiyo msimu ujao.
  Ligi Kuu itaendelea keshokutwa kwa mchezo mmoja pia, kati ya Azam FC na Stand United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Kwa Stand United ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 22 haina nafasi ya ubingwa na wala haimo kwenye hatari ya kushuka daraja, hivyo huo ni mchezo ambao hauwatii ‘presha’ hata kidogo.
  Lakini Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi zake 47 za mechi 20 katika mbio za ubingwa dhidi ya Yanga yenye pointi 50 za mechi 21 na Simba iliyo kileleni kwa pointi zake 54 za mechi 23 – inahitaji ushindi ili kujiimarisha.  
  Na baada ya kurejea Dar es Salaam jana kutoka Afrika Kusini ilikowachapa 3-0 wenyeji Bidvest Wist katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC imeingia kambini moja moja katika hosteli zake za Azam Complex, Chamazi kujiandaa na mchezo huo.
  Mabingwa watetezi, Yanga wao watarudi kwenye Ligi Kuu baada ya mchezo wao wa marudiano wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR ya Rwanda Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga walioifunga APR 2-1 katika mchezo wa kwanza Jumamosi mjini Kigali – waterejea kwenye Ligi Kuu Machi 23, wakiikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Taifa.
  Simba itaendelea kukimbizwa katika Ratiba ya Ligi Kuu kwa kucheza na Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LIGI KUU BARA YAZIDI KUNOGA, SPORTS NA MBEYA CITY KUKINUKISHA MKWAKWANI LEO, AZAM FC WANA STAND UNITED CHAMAZI JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top