• HABARI MPYA

  Thursday, March 10, 2016

  MIAKA 122 YA UPINZANI WA MAN UNITED NA LIVERPOOL YAHAMIA ULAYA LEO

  MIAKA 122 ya upinzani wa jadi wa Liverpool na Manchester United inaingia katika anga nyingine, wakati miamba hiyo itakapokutana katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya michuano ya Europa Uwanja wa Anfield.
  Baada ya mechi 194 za mashindano ya nyumbani, England baina ya timu hizo tangu mwaka 1894, upinzani wao sasa unahamia kwenye michuano midogo ya Ulaya kwa mara ya kwanza.
  Zote Liverpool na United hakuna kati yao mwenye uhakika wa kupata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kutokana na Ligi Kuu ya England kwa sababu hazina nafasi ya kumaliza ndani ya nne bora, hivyo zinahitaji kushinda Europa League ili kupata nafasi hiyo.
  Kocha Louis van Gaal akiwaandaa wachezaji wa Manchester United kwa mchezo wa usiku wa Alhamisi

  Kocha wa United yenye mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa, Louis van Gaal amesema kwamba klabu zote zipo sawa, akiwaambia Waandishi wa Habari katika Mkutano wa kabla ya mechi kwamba: "Unaishi katika zama zilizopita".
  "Mataji mangapi wanayo Liverpool sasa na mataji mangapi wanayo sasa Manchester United?"alihoji. "Ulikuwa wakati mwingine. Unatakiwa kuishi katika wakati huu. Haya yanatokea katika soka. Ni kawaida. Ni kawaida kwamba timu ilitawala kwa miaka 20 mfululizo kama mabingwa."
  Ikiwa sasa inashika nafasi ya sita katika Ligi Kuu ya England, United haijakata tamaa kumaliza ndani ya nne bora, lakini Van Gaal atakuwa katika wakti mgumu akitolewa na Liverpool.
  Mholanzi huyo ameshinda mechi zake zote nne zilizopita alizokutana na Liverpool yenye mataji matano ya Ligi ya Mabingwa, ikiwemo ushindi wa nyumbani na ugenini katika mechi za ligi msimu huu, na timu yake imezinduka hivi karibuni baada ya kushinda mechi nne mfululizo.
  Lakini kipigo cha 1-0 Jumapili kutoka kwa West Bromwich Albion kinawapunguzia pointi tatu katika nafasi ya kuwania kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, ikiwa imecheza mechi zaidi ya Manchester City inayoshika nafasi ya nne.
  Liverpool inazidiwa pointi tatu na United na mchezo mmoja mkononi baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Crystal Palace, ikitoka kulipa kisasi cha kufungwa kwa mikwau ya penalti na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi kwa kuwachapa 3-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu.
  Lakini wakati United bado inawania Kombe la FA, ikielekea kwenye mchezo wa Robo Fainali na West Ham United Uwanja wa Old Trafford Jumapili, michuano ya Europa League inabaki nafasi pekee kwa kocha wa Liverpool Jurgen Klopp kuwania taji msimu huu.

  Kocha Jurgen Klopp (katikati kulia) na wasaidizi wake, wakiwaelekeza mambo wachezaji wao kuelekea mechi na Manchester United

  'MAMA WA MICHEZO YOTE'
  Klopp ameiita mechi hiyo kama "Mama wa michezo yote".
  "Hizo mechi ni nyepesi, kwa sababu ni kubwa mno,"amesema Mjerumani huyo aliyemrithi Brendan Rodgers aliyefukuzwa Oktoba mwaka jana.
  "Huhitaji kufikiria kuhusu kutilia maanani, kwa sababu wazi unafikiria. Ni kubwa. Sihitaji kulinganisha michezo. Ikiwa unafanya kazi (Borussia) Dortmund, kama nilivyokuwa, na unacheza dhidi ya Schalke, haiwezekani kuzungumzia chochote kingine.
  "Ni kama hapa tu na ratiba hii. Kweli ni mchezo mkubwa. Natumai si mkubwa kuliko yote nikiwa kazini Liverpool, lakini ni muhimu sana,".
  Winga wa United, Jesse Lingard ataukosa mchezo huo kwa sababu atakuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano alizopewa katika mechi zote mbili wakiitoa kwa jumla ya mabao 6-3 FC Midtjylland ya Denmark kwenye raundi ilyotangulia.
  Wayne Rooney ataendelea kukosekana kutokana na maumivu ya goti, wakati mshambuliaji kinda wa miaka 18, Marcus Rashford, ambaye aliibuka kwa kishindo akifunga mabao mawili katika mechi ya kwanza kuchezea kikosi cha kwanza cha United, ikishinda 5-1 dhidi ya Midtjylland mwezi uliopita anatarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza Ywanja wa Anfield.
  Antonio Valencia anaweza kurejea kufuatia kupona maumivu ya mguu, lakini Ashley Young, Luke Shaw, Bastian Schweinsteiger na Phil Jones wataendelea kukosekana, wakati Adnan Januzaj na Timothy Fosu-Mensah ineligible wanatarajiwa kucheza.
  Kiungo Philippe Coutinho na mshambuliaji, Daniel Sturridge wanatarajiwa kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool baada ya kuanzia benchi wakishinda dhidi ya City na Palace.
  Nathaniel Clyne atachukua nafasi beki ya kulia kutoka kwa Jon Flanagan, ambaye hajasajiliwa kwenye kikosi cha Liverpoool cha  michuano ya Ulaya 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MIAKA 122 YA UPINZANI WA MAN UNITED NA LIVERPOOL YAHAMIA ULAYA LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top