• HABARI MPYA

  Monday, March 07, 2016

  JOHN BOCCO: KUWAFUNGA YANGA MFULULIZO SI MCHEZO!

  Na Adam Fungamwango, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Azam FC, John Raphael Bocco maarufu kwa jina la utani 'Adebayor' (pichani kulia) amesema kwamba si kazi rahisi kuwafunga mfululizo Yanga, lakini yeye ameweza kwa sababu amekuwa akijipanga vizuri kabla ya mechi hizo.
  "Si kazi rahisi, ispokuwa mimi nimekuwa najipanga sana kabla ya mechi na Yanga kwa sababu najua hata wao huwa wanajipanga kwa ajili yangu. Nakuwa nawasoma sana mabeki wao, makosa yao nayajua na mimi nikiingia uwanjani najua hata wanikabe vipi, lakini kuna wakati wataniachia mwanya nitafanya yangu,"amesema Bocco akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo.
  Bocco amesema Yanga ni timu nzuri na hakuna ubishi ndiyo wapinzani wao wakuu kwa sasa katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.   
  Bocco Jumamosi alifikisha mabao 10 aliyofunga kwenye mechi za Ligi Kuu pekee dhidi ya Yanga tangu Azam FC ilipopanda mwaka 2008, baada ya kufunga bao la pili katika sare ya 2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na Bocco sasa ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi tangu timu hizo zianze kupambana kwenye mechi za Ligi Kuu kuanzia msimu wa 2008/09.
  Alifunga bao lake la kwanza msimu wa 2009/10 Azam ikitoka sare ya bao 1-1, lingine lilikuwa ni la kufutia machozi timu hiyo ikikubali kipigo cha mabao 2-1 msimu huo huo wa 2009/10 kwenye mechi ya mzunguko wa pili.
  Bocco alifunga bao la tatu msimu wa 2010/11 likiwa bao pekee Azam ikiichapa Yanga bao 1-0, na bao la nne alilipata kwenye mechi ya mzunguko wa pili msimu huo huo Azam ikichapwa mabao 2-1.
  Msimu wa 2011/12 alifunga bao pekee Azam ikiichapa Yanga bao 1-0 na kuwa bao lake la tano, kabla ya kufunga mawili msimu huo huo, mechi ya mzuguko wa pili Azam ikiisasambua Yanga 3-1 na kuwa bao lake la saba.
  Alifunga moja na likiwa ni la nane msimu 2013/14 timu yake ikiiadhibu Yanga mabao 3-2, na msimu wa 2014/15 alifunga bao moja likiwa ni la kusawazisha timu hizo zilipotoka sare ya mabao 2-2 na kufikisha idadi ya magoli tisa, kabla ya kufunga bao lingine ya kusawazisha juzi timu hizo zikitoka sare ya 2-2 Jumamosi na kukamilisha mabao 10.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JOHN BOCCO: KUWAFUNGA YANGA MFULULIZO SI MCHEZO! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top