• HABARI MPYA

    Sunday, September 23, 2012

    MINZIRO AKATAA UKOCHA MKUU YANGA

    Minziro kulia akiwa Kocha wa Makipa Yanga, Mfaume Athumani

    Na Mahmoud Zubeiry
    KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Freddy Felix Isaya Kataraiya Minziro amesema kwamba hawezi kusema yuko tayari kuwa Kocha Mkuu wa kudumu wa klabu hiyo, kwa sababu jukumu hilo anaona litakuwa zito kwake, kulingana na uzito wa klabu yenyewe.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari jana baada ya mechi dhidi ya JKT Ruvu, ambayo aliiongoza Yanga kushinda 4-1, beki huyo wa zamani wa Yanga, alisema kwamba hawezi kuanza kutamba anatosha kuwa kocha Mkuu baada ya ushindi huo, kwa sababu ligi ni ndefu.  
    “Siwezi kusema natosha kuwa Kocha Mkuu, kwa sababu mambo ya mpira leo umeshinda, kesho kuna kufungwa, nachoweza kusema namshukuru Mungu tu kwa ushindi huu,”alisema mtaalamu huyo wa zamani wa mipira ya mkato wa ndizi ‘Banana chop’.  
    Akiuzungumzia ushindi huo, Minziro alisema umetokana na ushirikiano baina yake na wachezaji, kwani alipewa jukumu la kukaimu ukocha mkuu ghafla tu jana, baada ya kufukuzwa kwa aliyekuwa bosi wake, Mbelgiji, Tom Saintfiet.
    Aidha, Minziro alisema kwamba ushindi huo umetokana na timu kutumia vema nafasi ilizopata jana, tofauti na ilivyokuwa kwenye mechi mbili zilizopita, dhidi ya Prisons mjini Mbeya waliyotoka sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar waliyofungwa 3-0 Morogoro.
    Alisema pia hali nzuri ya Uwanja wa Taifa, tofauti na wa Sokoine mjini Mbeya na Jamhuri, Morogoro nayo ilichangia ushindi wa jana.
    Kuelekea mechi na watani wa jadi, Simba SC,Oktoba 3, mwaka huu, Minziro maarufu kwa jina la utani Majeshi, alisema kwamba itakuwa ngumu, lakini kwa kuwa hii si mara yak wake kuachiwa timu, atakabiliana na jukumu hilo.
    Yanga jana ilipata ushindi wa kwanza ndani ya mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hadi mapumziko Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Nahodha, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ dakika ya nne na Didier Kavumbangu dakika ya 31, mabao yote yakitokana na kazi nzuri ya kiungo mshambuliaji Simon Msuva.
    Bao la kwanza ulikuwa mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Niyonzima, baada ya Msuva kuangushwa karibu kabisa na eneo la hatari la JKT Ruvu na bao la pili dogo huyo aliyesajiliwa kutoka Moro United iliyoshuka daraja, alimpa pasi mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kavumbangu.
    Kipindi cha pili, Yanga walirudi tena kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 52, mfungaji Simon Msuva kabla ya Didier Kavumbangu kufunga la nne dakika ya 65.
    JKT ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 68 mfungaji Credo Mwaipopo.
    Katika mchezo wa leo, Yanga ilicheza vizuri, wachezaji wakionana kwa pasi nzuri ndefu na fupi, tofauti na ilivyokuwa kwenye iliyopita mjini Morogoro, ambako walifungwa 3-0 na Mtibwa Sugar.
    Ikumbukwe mechi ya kwanza, Yanga ililazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons mjini Mbeya.
    Yanga leo ilicheza chini ya kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro, baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet kusitishiwa mkataba jana usiku, kufuatia kutofautiana na uongozi.
    Kikosi cha Yanga jana kilikuwaYaw Berko, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan/Shamte Ally, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu/Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Simon Msuva.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MINZIRO AKATAA UKOCHA MKUU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top