• HABARI MPYA

  Saturday, September 22, 2012

  YANGA NA JKT RUVU LEO KATIKA MECHI YA USHINDI LAZIMA TAIFA

  Saintfiet akiwapungia mikono mashabiki wa Yanga SC wakati akiingia Uwanja wa jamhuri kwenye mechi iliyopita, kumbe alikuwa anawaaaga.

  Na Mahmoud Zubeiry
  MABINGWA wa soka Afrika Masharikia na Kati, Yanga SC leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Hiyo itakuwa moja kati ya mechi nne za leo za ligi hiyo, nyingine zikiwa ni kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, JKT Oljoro na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha na Coastal Union na Toto Africans kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu kwa sababu timu zote, zilifungwa katika michezo yao iliyopita, Yanga ikichapwa 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Mtibwa Sugar na JKT ikitundikwa 2-0 na mabingwa watetezi Simba SC.
  Angalau, JKT ilivuna pointi tatu kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting kwa ushindi wa 2-1 Uwanja wa Chamazi, lakini Yanga hata mechi yake ya kwanza ya ligi hiyo, ililazimishwa sare ya bila kufungana Prisons mjini Mbeya.
  Katika mchezo wa leo, Yanga inatarajiwa kuongozwa na kocha wake Msaidizi, Freddy Felix Minziro, kufuatia kutupiwa virago kwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet jana usiku, baada ya kutofautiana sera na uongozi.
  Saintfiet ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu tangu ajiunge nayo Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi hizo amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
  Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi. 
  Wachezaji wa Yanga watacheza mechi ya leo kwa shinikizo, kwa sababu uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Yussuf Mehboob Manji unaonekana kucharuka hivi sasa na kuwa tayari kuchukua maamuzi magumu, baada ya timu kuanza vibaya katika mechi mbili za awali za ligi hiyo.
  Jana, uongozi wa Yanga ya Dar es Salaam, ulitangaza kuisimamisha kazi Sekretarieti nzima ya klabu, akiwemo Katibu Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu, kutokana na kile ilichoeleza utendaji usioridhisha.
  Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, kwamba maamuzi hayo yamefuatia kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika tangu saa 5:30 hadi saa 9:30 jioni jana.
  Wengine waliokumbwa na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu mengine.
  Baada ya kuondolewa sekretarieti hiyo, sasa beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Lawrence Mwalusako atakaimu nafasi ya Katibu wa klabu hiyo, wakati kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Johnson Chambua atakuwa Meneja mpya wa klabu hiyo.
  Nafasi nyingine za Mhasibu mpya, iliyoachwa wazi na Philip Chifuka itakuwa chini ya dada mmoja, aliyetajwa kwa jina moja tu, Rose aliyekuwa akifanya kazi ofisi hiyo kwa muda mrefu, wakati Msemaji wa klabu iliyoachwa wazi na Louis Sendeu, inaelezwa atapewa mdogo wa mke wa Ridhiwani Kikwete, aliyehesabu kura za Abdallah Bin Kleb katika uchaguzi mdogo wa klabu, Julai 14.
  Mapema kabla ya kutupiwa virago jana, kocha Saintfiet alitaja wachezaji 18 wa kucheza mechi ya leo, akimteka mshambuliaji Said Bahanuzi, mfungaji bora wa Kombe la Kagame, lakini baada ya mabadiliko hayo hakuna hakika kama kikosi kitakuwa kile kile.
  Wachezaji aliowateua Mtakatifu Tom ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan,  Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
  Aliwataja viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Rashid Gumbo, Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza na ambao hawamo kwenye programu ya kesho ni kipa Said Mohamed, mabeki Nsajigwa Shadrack, Job Ibrahim, viungo Frank Domayo, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega, na Issa Ngao wa Yanga B anayekomazwa kikosi cha kwanza na mshambuliaji Said Bahanuzi.
  Mechi nyingine za ligi zitapigwa kesho, Mgambo JKT wakimenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Simba SC na Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na African Lyon na Prisons Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.


  MSIMAMO WA LIGI KUU BARA

                              P    W  D   L    GF       GA      GD      P
  Simba SC             2    2    -     -     5          -           5          6
  Mtibwa Sugar       2    1    1    -     3          -           3          4
  Azam FC              2    1    1    -     2          1          1          4
  Coastal                 2    1    1    -     2          1          1          4
  Ruvu Shooting      2    1    -     1    3          3          -           3
  JKT Ruvu              2    1    -     1    2          3          -1        3
  African Lyon          2    1    -     1    1          3          -2        3
  Toto African           2    -     2    1    3          2          1          2
  JKT Oljoro             2    -     2    1    1          -           -           2
  Prisons                  2    -     2    -     1          1          -           2
  Polisi Moro             2    -     1    1    -           1          -1        1
  Kagera Sugar        2    -     1    1    -           1          -1        1
  Yanga SC              2    -     1    1    -           3          -3        1
  JKT Mgambo         2    -     -     2    1          3          -2        0 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA NA JKT RUVU LEO KATIKA MECHI YA USHINDI LAZIMA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top