• HABARI MPYA

    Sunday, September 30, 2012

    KUELEKEA PAMBANO LA WATANI; SIWEZI KUSUBIRI KUWAONA KIEMBA NA KAZIMOTO V CHUJI NA NIYONZIMA

    Msuva kulia na Chuji kushoto

    Na Mahmoud Zubeiry
    SIKU moja niliandika, namna amabvyo Mrisho Ngassa na Christopher Edward huwa wanaelewana wakicheza pamoja mazoezini Simba na haikuchukua muda kocha Milovan Cirkovick akaanza kuwapanga pamoja kwenye mechi wawili hao.
    Wote wawili wana kasi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Wadanganyifu na wahangaikaji uwanjani. Ni watu ambao hutakiwi kuwasahau hadi kipyenga cha mwisho na hata kuwadhibiti tu ni kazi, kwa sababu hawachoki na hawakati tamaa.
    Kuelekea mpambano wa watani wa jadi Jumatano, naamini Yanga watakuwa wana kazi kubwa mbele ya ‘viberenge’ hivi. Lakini upande wa pili, Yanga wana dogo mmoja anaitwa Simon Msuva anacheza vizuri, lakini hana ushirikiano mzuri na Hamisi Kiiza ‘Diego’.
    Msuva na Kiiza wote wana kasi na wanajua kufunga, lakini unaweza kuona Diego anawatengenezea sana nafasi wenzake, ila yeye zaidi anafunga kwa juhudi zake. Katika mechi na JKT Ruvu, Kiiza alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, ila Msuva baada ya kuwakimbia mabeki wa timu hiyo akiwa wingi ya kulia ndani kidogo alilazimisha kufunga mwenyewe japo hakuwa kwenye nafasi nzuri na akakosa.
    Kiiza alisikitika mno na haya ni mambo ambayo yanasababisha utofauti wa Edward na Ngassa dhidi ya Kiiza na Msuva.    

    NGASSA NA YONDAN:
    Kumbuka, tayari kuna kumbukumbu ya Kevin Yondan kuwa njia ya Ngassa. Hiyo ni wakati ambao Ngassa alikuwa anacheza Yanga na Yondan yupo Simba. Mmoja wa watu waliomsababishia Yondan kutoaminiwa Simba ni Ngassa- aliwahi kumpiga chenga moja kali hadi akaanguka na ‘kulala kabisa’ katika mechi ya watani.
    Lakini sasa Yondan yupo Yanga atakuwa akimkaba Ngassa wa Simba. Ndiyo, Ngassa wa sasa anacheza pembeni, lakini anaingia sana ndani katika kushambulia na hivyo ndivyo inavyotakiwa na Yondan kama mtu wa mwisho kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, lazima tu atakumbana na mtihani wa Mrisho Jumatano.
    Achana na hilo, Ngassa anacheza vizuri sana pale mbele akiiongoza timu, kwa kutoa pasi na kuombea upande mwingine na pamoja na kwamba amefunga bao moja tu kwenye mechi nne za Ligi Kuu, lakini bado mchango wake mkubwa Simba.
    Edward ana kipaumbele cha ziada cha kudharauliwa, kuchukuliwa kama mtoto mdogo tu na kwa hilo aliifungia Simba bao la ushindi kwenye mechi na Ruvu Shooting, mabeki wa timu hiyo ya Charles Boniface Mkwasa waliwawekea ulinzi zaidi, akina Ngassa na Okwi lakini matokeo yake dogo huyo mfungaji bora wa Kombe la BancABC akashinda mechi.

    KIIZA NA CHOLLO
    Nassor Masoud ‘Chollo’ ndiye beki tegemeo la Simba kwa sasa katika beki ya kulia tangu msimu umeanza, lakini huyu msimu uliopita alikuwa uchochoro wa Kiiza hususan katika fainali ya Kombe la Kagame msimu uliopita.
    Na Simba ilibidi wamrudishe benchi wakati fulani na kumpa Shomary Kapombe jukumu la kucheza beki ya kulia. Ila, kutokana na tatizo la beki ya kati, imebidi Kapombe aingizwe katikati na Chollo arudi kucheza wingi ya kulia chini.
    Kweli Chollo anaonekana yuko vizuri kwa sasa anakaba na kusaidia mno mashambulizi, lakini je amefanya hivyo dhidi ya wachezaji wa aina gani, ya Kiiza? Tutajua Jumatano.
    Nyosso kulia


    NYOSSO ‘UGONJWA WA MOYO’, LAKINI HATA CANNAVARO ‘RUSHA ROHO’
    Beki ya kati Simba inatia sana hofu mashabiki wa timu yake, kama inaweza kuwadhibiti washambuliaji hatari wa Yanga akina Said Bahanuzi, Didier Kavumbangu au hata akipangwa Jerry Tegete.
    Zaidi ni Juma Said Nyosso ambaye kwa sasa anacheza kwa pamoja na Shomary Kapombe. Watu hawana wasiwasi na Kapombe, ila wanakosa usingizi kwa sababu ya Nyosso. Kweli, Nyosso ni ‘ugonjwa wa moyo’, lakini hata Yanga nao wanapaswa kujua kwamba Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hajacheza vema katika mechi zote za Simba msimu uliopita na kiwango chake kimeshuka kidogo.
    Inatokea hiyo kwa wachezaji, haswa wa safu ya ulinzi, kwani hata Rio Ferdinand yule siyo huyu- hivyo hakuna ajabu kwa Cannavaro. Sunzu aling’ara mno kwenye mechi na Yanga msimu uliopita, kwa sababu ya ubutu wa beki ya kati ya Yanga iliyoongozwa na Cannavaro msimu uliopita.
    Je, safari hii akiwa na Kevin Yondan na hii ikiwa mechi yao ya kwanza dhidi ya Simba kucheza tutarajie nini? Ila hadi sasa, kama watu wanasema Nyosso ugonjwa wa moyo, basi hata Cannavaro rusha roho vile vile.
    Niyonzima anafanya safari upande wa Chollo

    HAPA NASUBIRI KUJIONEA, KIEMBA NA KAZIMOTO V CHUJI NA NIYONZIMA;
    Sijui Milovan atapangaje safu yake ya kiungo, lakini kuna uwezekano mkubwa kiungo mkabaji akawa Amri Kiemba na juu yake akacheza Mwinyi Kazimoto, ingawa kama nilivyosema sijui, kwa sababu ana viungo wengine akina Jonas Mkude anaweza kucheza chini, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Salim Kinje wanaweza kucheza juu wote.
    Yanga pia nako chini kuna Frank Domayo, dogo anayeinukia vizuri, lakini bila shaka Athumani Iddi ‘Chuji’ ndiye ataanza pale chini na juu ni Haruna Niyonzima ingawa wapo viungo wengine kama Nizar Khalfan na Juma Seif ’Kijiko’.
    Wote hawa ni viungo wataalamu na wenye wazoefu- ni burudani kiasi gani tutarajie iwapo wachezaji hawa wote wanne watacheza kwa viwango vyao?
    Akuffo kulia akishangilia, nyuma yake Nyosso

    MSHAMBULIAJI BORA ATAJULIKANA SIKU HIYO;
    Simba kuna mzalendo mmoja tu kwenye safu ya ushambuliaji Abdallah Juma ‘Dullah Mabao’ na wageni wawili, Daniel Akuffo na Felix Sunzu, wakati Yanga kuna wazalendo wawili na mgeni mmoja, Jerry Tegete, Said Bahanuzi na Didier Kavumbangu.
    Kuna uwezekano mkubwa, Kiiza na Msuva wakicheza pembeni- Bahanuzi na Kavumbangu wakaanza pale mbele ya mdomo wa lango na kwa Simba kama hawatapangwa Sunzu na Akuffo waanze pamoja, basi mmoja wao ataanza na Ngassa na kufanya idadi ya viungo zaidi uwanjani upande wa timu hiyo.
    Kumbuka hata Edward Christopher anaweza kucheza mbele ya mdomo wa lango, lakini bado sijui kwa nini Dullah Mabao haaminiwi Simba wakati dogo anaweza sana tu na analijua goli?
    Kiemba na Kazimoto wakimpongeza Sunzu
    Yote kwa yote, yeyote atakayepangwa acheze na yeyote, ila Jumatano ndio tutawajua washambuliaji hatari waliosajiliwa na miamba hiyo ya soka nchini msimu huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUELEKEA PAMBANO LA WATANI; SIWEZI KUSUBIRI KUWAONA KIEMBA NA KAZIMOTO V CHUJI NA NIYONZIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top