• HABARI MPYA

  Saturday, September 22, 2012

  HANS POPPE: TFF WANAOGOPA TUKIPELEKA FIFA SUALA LA TWITE, YONDAN WATAAIBIKA NDIO MANA WANABANA HATI YA HUKUMU

  Hans Poppe

  Na Mahmoud Zubeiry
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba hadi sasa klabu yake haijapata barua ya hukumu ya pingamizi zao dhidi ya wachezaji Mbuyu Twite na Kevin Yondan kuidhinishwa kuchezea Yanga kutoka Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba kutokana na kutopatiwa hati hiyo ya hukumu, wanashindwa kukata rufaa, Mahakama ya Usuluhishi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), CAS.
  “Tumekwishawaandikia barua ya kuwaomba hati ya hukumu, lakini bado hadi leo hawajatupa, sasa tunashindwa kuelewa nini lengo lao, tunafikiria wanajua tukikata rufaa CAS tutashinda, sasa wamejawa hofu na wanaogopa kutoa hukumu kwa maandishi,” alisema Hans Poppe.
  Septemba 10, mwaka huu Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa ilitoa maamuzi ambayo hayakuwaridhisha walalamikaji, Simba SC juu ya Twite na Yondan na sasa wanataka kulipeleka suala hilo CAS.
  Kamati hiyo, iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya kuingia mkataba na Yondan na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati hiyo.
  “Kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
  Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa.
  Kuhusu suala la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali.
  Hata hivyo, alisema kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
  Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
  Siku 21 walizopewa Yanga kurudisha fedha za Twite alizochukua Simba, zinamalizika Oktoba 3, mwaka huu siku ambayo watani hao wa jadi katika soka ya Tanzania, watamenyana katika mchezo wa Ligi Kuu, mzunguko wa kwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE: TFF WANAOGOPA TUKIPELEKA FIFA SUALA LA TWITE, YONDAN WATAAIBIKA NDIO MANA WANABANA HATI YA HUKUMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top