• HABARI MPYA

  Monday, September 24, 2012

  MANJI KUJENGA UWANJA WA KISASA JANGWANI, UTAKUWA BAAB KUBWA TANZANIA NZIMA HAKUNA

  Uwanja mpya wa Kaunda utakavyokuwa

  Na Mahmoud Zubeiry
  KLABU ya Yanga ipo katika mkakati wa kujenga Uwanja mpya wa kisasa sambamba na kukarabati jengo la makao makuu ya klabu, liliopo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
  Habari ambazo, BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba tayari mkandarasi amekwishaptikana na amefikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo.
  Habari zaidi zinasema, Uwanja mpya wa Kaunda utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 40,000 na eneo la maegesho ya magari yasiyopungua 1,000 na zoezi la ujenzi wa Uwanja huo, litaanza kabla ya tarahe ya mwisho ya mwaka huu.
  Inadaiwa mradi huo, utafadhiliwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji, ambaye amedhamiria kufanya mambo mengine makubwa, kubadilisha kabisa sura na hadhi ya klabu hiyo, ili viendane na klabu nyingine kubwa Afrika.
  Wachezaji wakiwa mazoezini Uwanja wa Kaunda wa sasa
  Manji amekuwa mfadhili wa Yanga tangu mwaka 2006, wakati klabu hiyo ikiwa chini ya Mwenyekiti, Francis Mponjoli Kifukwe na baada ya kuona jitihada zake za kuifanya Yanga iwe ya hadhi ya juu zinakwamishwa na viongozi, Julai 14, mwaka huu akaamua kujitosa kugombea Uenyekiti wa klabu hiyo, katika uchaguzi mdogo.
  Ili kuhakikisha anapata timu nzuri ya kufanya nayo kazi, Manji aliwapigania Clement Sanga, Abdallah Bin Kleb, Mussa Katabaro, George Manyama na Lameck Nyambaya aingie nao madarakani.
  Katika timu hiyo, iliyopewa jina ‘Jeshi la Miamvuli’ Sanga alifanikiwa kuwa Makamu Mwenyekiti, Bin Kleb, Manyama na Katabaro wakipata Ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wakati Nyambaya alizidiwa kura na Aaron Nyanda.
  Uwanja wa Kaunda na jengo la sasa la klabu, vilijengwa kwa nguvu za wanachama wake, chini ya Mwenyekiti wake wa kwanza, Mangara Tarbu miaka ya 1970 pamoja na msaada wa rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amaan Karume.
  Ingawa historia inasema Yanga ilizaliwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
  Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938 ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
  Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs, vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina Jangwani.
  Unavyoonekana Uwanja wa Kaunda hivi sasa
  Ndani ya kipindi kifupi tu, timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo. Miongoni mwa waliovutika na uanachama wa klabu hiyo ni Tarbu Mangara (sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926, walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
  Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
  Hiki ndio choo cha Uwanjda wa Kaunda 
  Baada ya mkutano huo, timu hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana Jangwani hao.
  Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo zaidi. Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Taliana.
  Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
  Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
  Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema Yanga.    
  Miongoni mwa wachezaji wa mwanzoni kabisa wa Yanga ni kipa Taha Athumani, Saidia Msafiri na Jamil Ramadhan. Waliofuatia walikuwa ni kipa Abdulhamid Ramadhan, aliyewika na kuisaidia Tanganyika kutwaa Kombe la Gossage (sasa Challenge) katika miaka ya 1949 na 1950.
  Hili ndio jukwaa la sasa la Uwanja Kaunda
  Lakini mbali na jengo la makao makuu ya klabu na Uwanja wa Kaunda, Yanga pia ina nyumba Mtaa wa Mafia, ambayo kwa muda mrefu imetelekezwa, ingawa wanaweza kuikarabati kwa kujenga jengo la kisasa la kitegauchumi, katika Kariakoo mpya iliyosheheni maghorofa.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MANJI KUJENGA UWANJA WA KISASA JANGWANI, UTAKUWA BAAB KUBWA TANZANIA NZIMA HAKUNA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top