• HABARI MPYA

  Sunday, September 23, 2012

  KOCHA JKT APAGAWA NA NNE ZA YANGA

  Charles Kilinda

  Na Mahmoud Zubeiry
  KOCHA Mkuu wa JKT Ruvu, Charles Kilinda jana alikacha kuzungumzia kipigo cha mabao 4-1 walichopewa na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kumuachia msaidizi wake, Azishi Kondo.
  Tofauti na ilivyo ada yake, kiungo huyo wa zamani wa Yanga, Kilinda ambaye huwa mwepesi kuzungumza wakati wowote, kabla na baada ya mechi, jana hakuingia kabisa kwenye chumba cha mikutano.
  Msaidizi wake, beki wa zamani wa timu hiyo, Kondo alizungumzia kipigo hicho kama matokeo ya soka na zaidi akasema kilichangiwa na kukosekana kwa wachezaji wake muhimu, waliokuwa majeruhi.
  “Mabao manne ni mengi kwa kweli, imetokana na makosa, ndiyo mambo ya mpira, tumefungwa kwa sababu za kisoka,”alisema mdogo huyo wa Kocha Msaidizi wa Coastal Union, Habib Kondo.
  Mdogo huyo wa beki wa zamani wa Simba SC, Adolph Kondo alisema kwamba wachezaji kadhaa waliocheza mechi iliyopita ambayo walifungwa mabao 2-0 na Simba, kama kipa namba moja, Shaaban Dihile, Amos Mgisa na George Minja jana wote walikuwa majeruhi.
  Kuhusu madai kwamba, JKT imeshuka kiwango kwa kusajili ‘wazee’ kama Credo Mwaipopo, Kondo alisema; “Si kweli kwamba Credo ni mkongwe, hapana, Credo bado mdogo tu, sema alicheza Yanga, klabu kubwa, ni mchezaji mzuri, alikuwa nje, karudi, tumemsajili na leo kacheza vizuri,”alisema.
  Credo aliyecheza Yanga 2006 hadi 2008, akiwa anaibukia kisoka nchini, baada ya hapo alikwenda Sweden kucheza soka ya kulipwa hadi aliporejea msimu huu na kusaini timu hiyo ya jeshi.
  JKT Ruvu jana ilipoteza mechi ya pili ya Ligi Kuu kati ya tatu, ikifungwa 4-1 na kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Hadi mapumziko Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Nahodha, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ dakika ya nne na Didier Kavumbangu dakika ya 31, mabao yote yakitokana na kazi nzuri ya kiungo mshambuliaji Simon Msuva.
  Bao la kwanza ulikuwa mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Niyonzima, baada ya Msuva kuangushwa karibu kabisa na eneo la hatari la JKT Ruvu na bao la pili dogo huyo aliyesajiliwa kutoka Moro United iliyoshuka daraja, alimpa pasi mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kavumbangu.
  Kipindi cha pili, Yanga walirudi tena kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 52, mfungaji Simon Msuva kabla ya Didier Kavumbangu kufunga la nne dakika ya 65.
  JKT ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 68 mfungaji Credo Mwaipopo.
  Kikosi cha JKT jana kilikuwa; Said Mohamed, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Damas Makwaya, Charles Timoth, Ally Khan, Haroun Adolf, Said Ahmed ‘Ortega’/Jimmy Shoji, Omar Changa/Furaha Tembo, Hussein Bunu na Sosstenes Manyasi/Credo Mwaipopo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA JKT APAGAWA NA NNE ZA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top