• HABARI MPYA

    Sunday, September 23, 2012

    KWAHERI MTAKATIFU TOM, HIYO NDIYO YANGA



    SIKU 80, mechi 14 na taji moja, vimetosha kukamilisha historia ya mtaalamu wa soka kutoka Ubelgiji, Tom Saintfiet ndani ya klabu ya Yanga.
    Na Mahmoud Zubeiry
    Hiyo inafuatia kufukuzwa kwa Kocha huyo juzi usiku na nafasi yake sasa anakaimu Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro hadi hapo atakapopatikana kocha mwingine.
    Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia Waandishi wa Habari jana asubuhi, makao makuu ya klabu, makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani kwamba, matokeo mabaya ndio yamefanya Saintfiet asitishiwe mkataba.
    Aidha, Sanga alikanusha madai kwamba eti kocha huyo amefukuzwa baada ya kutofautiana na Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji.
    “Timu ilipokwenda Mbeya, ikatoka sare na Prisons akalalamikia huduma, lakini sisi taarifa tulizozipata, yeye alikwenda kulewa na wachezaji. Kuna mapungufu mengine mengi, ambayo hatuwezi kusema hadharani.
    Kwa mfano timu ilipotoka Mbeya, tulitaka iende moja kwa moja Morogoro, yeye akalazimisha timu irudi Dar es Salaam, tena iende tena Morogoro. Wachezaji wakachoka sana na hii tunaamini ilichangia hata kufungwa na Mtibwa.
    Timu iliporudi kutoka Morogoro, tukaamua iingie kambini, yeye akapinga akisema timu kubwa kama Barcelona Ulaya, hazikai kambini, yaani anataka atupangie kazi sisi, tukaona huyu mtu haendani na maadili ya uongozi na hatufai, tukaamua kusitisha mkataba wake,” alisemsa Sanga.  
    Saintfiet ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu ndani ya siku 80 tangu ajiunge nayo Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi hizo amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
    Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi. 
    Pamoja na kufukuzwa kwa kocha, Yanga imemtangaza rasmi beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Lawrence Mwalusako kukaimu nafasi ya Katibu wa klabu hiyo na Dennis Oundo kuwa kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.
    Hatua hiyo, inafuatia kusimamishwa kazi kwa Sekretarieti nzima ya klabu, akiwemo Katibu Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu, kutokana na kile ilichoeleza utendaji usioridhisha.
    Wengine waliokumbwa na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu mengine.
    Mbali na Mwalusako na Oundo, kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Johnson Chambua anatajwa kupewa nafasi ya Umeneja, wakati nafasi ya Msemaji wa klabu iliyoachwa wazi na Louis Sendeu, inaelezwa atapewa mdogo wa mke wa Ridhiwani Kikwete, aliyehesabu kura za Abdallah Bin Kleb katika uchaguzi mdogo wa klabu, Julai 14.
    Ni ukweli usiopingika kwamba wana Yanga wengi wamesikitishwa na uamuzi wa kufukuzwa kwa Mbelgiji huyo, siku 80 tangu apokewe kwa sherehe kubwa akiwasili nchini kwa ajli ya kufanya kazi Jangwani.
    Wanakumbuka walivyosherehekea naye ubingwa wa Kagame. Wanakumbuka alivyokuwa akiiongoza vema timu hiyo na zaidi wanakumbuka ahadi zake, ambazo hajapewa fursa ya kuzitimiza, ikiwemo ubingwa wa Afrika.
    Uongozi wa Yanga unawajibika kwa wanachama na mwisho wa siku juu ya uendeshwaji wa timu, hakuna anayeweza kuwaingilia kwa sababu hilo ndilo jukumu walilopewa na wenye timu yao.
    Tom ameondolewa. Kocha mcheshi, asiye mwoga mbele ya vyombo vya habari, na ambaye katika kipindi kifupi cha kuwapo kwake nchini alijiengea umaarufu mkubwa kwa kazi nzuri na ushirikiano pia na wadau.
    Kwaheri Tom, kocha ambaye akiwa Ethiopia alipewa jina la utani Mtakatifu na vyombo vya habari kutokana na jinsi alivyokubalika, wakati akiifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo.
    Tumesikia sababu za uongozi kumfuta kazi Tom, na hata bila ya kuzijadili huu ni mwendelezo wa desturi ya Yanga kutodumu na makocha. Sijui kwa sababu gani.
    Tangu mwaka 1991, Saintfiet anakuwa kocha wa 18 kutupiwa virago Yanga na katika kipindi chote hicho ni makocha watatu tu, waliorudishwa kazini, baada ya kuondoka, ambao ni Syllersaid Mziray (sasa marehemu), Mmalawi Jack Chamangwana na Mserbia Kostadin Papic.
    Baadhi ya makocha waliamua kuondoka wenyewe, lakini wengi wao walifukuzwa na tawala mbalimbali zilizopita katika klabu hiyo katika kipindi chote hicho.
    Kwa nini nimeanzia 1991, ndicho kipindi ambacho vurugu vurugu za kufukuza makocha zilipoanza katika klabu hiyo, tofauti na miaka ya nyuma tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1939.
    Mapema mwaka 1991, Yanga ilimchukua kocha maarufu zamani nchini, Syllersaid Salmin Kahema Mziray, ambaye aliondoka kwa watani wa jadi, Simba SC, baada ya kushushwa cheo kutoka Simba A hadi Simba B.
    Mziray aliiongoza Yanga kwa miaka miwili, akiwa anasaidiwa na Charles Boniface Mkwasa na akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Bara na Muungano mfululizo, sambamba na kuwafikisha Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, ambako walifungwa kwa matuta na watani wa jadi, Simba SC.
    Lakini baada ya hapo, marehemu Mziray aliondoka Yanga kutokana na kupata ofa nzuri kutoka Pan African, wakati huo ikiwa inafadhiliwa na Murtaza Dewji, ambaye alikuwa anaipigania irejee Ligi Kuu.
    Yanga iliajiri tena kocha wa kigeni baada ya muda mrefu, ikimleta Mrundi, Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ 1993 (sasa marehemu) ambaye aliendelea kufanya kazi na Mkwasa na katika mwaka wake wa kwanza, akaiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda.
    Tauzany aliporejea katika Ligi Kuu akaendelea vizuri na kazi, lakini haikuchukua muda akaingia kwenye mgogoro na mfadhili wa klabu hiyo wakati huo, Abbas Gulalamli (sasa marehemu).
    Tauzany alitumia vyombo vya habari kupambana na Gulamali na ilifikia hadi akawa anachafua jina lake kwa kusema anafanya biashara haramu. Ilikuwa vita kali na mbaya zaidi hata Mrundi hiyo alikuwa anakubalika mbele ya wanachama, hivyo kumfukuza ikawa tabu.
    Alichokifanya Gulamali, akamrejesha kocha ambaye alifanya kazi na kupendwa mno Yanga, Tambwe Leya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye awali alifanya kazi mwaka 1975 na 1976, akiiwezesha Yanga kuifunga Simba katika mechi ya kihistoria Nyamagana kabla ya kuipa Kombe la kwanza la Kagame 1975, kwa kuwafunga hao hao Simba 2-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Tambwe alitua nchini mwishoni mwa mwaka 1994 na jukumu lake alilopewa ni Ukurugenzi wa Ufundi, ambapo yeye akaamua kutengeneza timu nzuri ya vijana, iliyopewa jina Black Stars.
    Tauzany na kikosi cha Yanga chenye mastaa kibao nchini wakati huo, akafungwa mabao 4-1 na Simba SC na hapo ndipo timu nzima na kocha wao wakafukuzwa, wakabaki wachezaji saba tu ambao waliunganishwa na yosso wa Tambwe kutengeneza kikosi kipya, kilichofanya vizuri hadi kufika Robo Fainali ya Kombe la Washindi 1996.
    Tambwe naye akaondolewa kwa visa na badala yake akaajiriwa kocha mzalendo, Sunday Burton Kayuni 1997 ambaye naye pia hakudumu, kwani alikfukuzwa na akaajiriwa kocha wa muda kutoka Uingereza, Steve McLennan mwaka huo huo 1997.
    McLennan, kocha Mzungu wa kwanza mimi kufanya naye kazi Yanga, aliondolewa naye na nafasi yake akakaimu kwa muda aliyekuwa Msaidizi wake, Juma Pondamali ‘Mensah’.
    Siwezi kusahau siku alipofukuzwa McLennan, alimfuata msaidizi wake ambaye aliachiwa timu na kumuuliza; “Juma nani ni kocha mzuri, mimi au wewe?” Pondamali akawa anacheka tu, wapo kwenye basi timu inatoka Zanzibar kwenye mechi za Ligi ya Muungano.  
    Yanga ikaajiri kocha wa muda, ambaye alikuwa hajulikani kabisa, Tito Oswald Mwaluvanda (sasa marehemu) ambaye katika kujikosha kwa wanachama, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Rashid Ngozoma Matunda (sasa marehemu pia) akawa anamtambulisha kama Msimamizi wa mazoezi, wakati timu inatafuta kocha.
    Msimamizi wa mazoezi alichukua ubingwa wa Ligi Kuu na Ligi ya Muungano 1998, tena akiweka rekodi ya ushindi mnono zaidi katika Ligi ya Bara, mabao 8-0 waliyoifunga Kagera Shooting Stars (sasa Kagera Sugar), tena ikiwa inafundishwa na kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo, Zacharia Kinanda ‘Arrigo Sachi’ (sasa marehemu), Edibilly Jonas Lunyamila akifunga mabao matano peke yake.
    Mungu amrehemu Kinanda, lakini siku hiyo Lunyamila alimfikishia ujumbe, kwani kocha huyo alikuwa hamtaki Eddy katika timu ya taifa- hivyo zile bao tano alizofunga ilikuwa ujumbe tosha, kwamba alikuwa anakosea.
    Kana kwamba hiyo haitoshi, Mwaluvanda aliifikisha Yanga hadi hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, akiweka rekodi mbili kuifanya hiyo iwe klabu ya kwanza Tanzania kucheza hatua hiyo, yeye kuwa kocha wa kwanza mzalendo na wa mwisho hadi sasa kuifikisha timu katika hatua hiyo.
    Lakini pamoja na yote, mwaka 1998 mara tu baada ya Yanga kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, marehemu Mwaluvanda aliyekuwa anasaidiwa na Freddy Felix Isaya Kataraiya Minziro ‘Majeshi’ wakaondolewa wote na akaajiriwa kocha kutoka DRC, Raoul Jean Pierre Shungu aliyeingia na msaidizi wake, Abeid Mziba ‘Tekero’.
    Hii ilimuuma sana Mwaluvanda, kwa sababu ili kuingia hatua ya makundi ilibidi azitoe Rayon ya Rwanda iliyokuwa inafundishwa na Shungu na baadaye Coffee ya Ethiopia, lakini marehemu akawa anasema afadhali angeletwa kocha mwingine, si yule ambaye ameitoa timu yake kwenye mashindano. Wakubwa wakishaamua huwezi kupingana nao.
    Shungu aliipa Yanga Kombe la tatu la Kagame, katika michuano iliyofanyika mjini Kampala, Uganda 1999, lakini mwaka 2000 akaondolewa na akaajiriwa Charles Boniface Mkwasa ‘Master’, ambaye naye mwishoni mwa mwaka 2001, akatupiwa virago pia.
    Tangu 2002 hadi sasa ni miaka 10 tu, lakini katika kipindi hicho Yanga imefundishwa na makocha 11, tena wengine wakifukuzwa na kurudishwa kwenye kipindi hicho.
    Alipoondolewa Master Mkwasa, akaajiriwa Mmalawi Jack Lloyd Chamangwana ambaye mwaka 2003, alifukuzwa na mwaka 2004 akaajiriwa kocha kutoka DRC, Jean Polycarpe Bonghanya ambaye naye hakudumu, mwaka huo huo akaondolewa na kurudishwa Syllersaid Mziray.
    Marehemu Mziray alikuwa anasoma ishara za nyakati tu, naye alipoona upepo unaelekea kuwa mbaya akamuachia timu aliyekuwa Msaidizi wake, Kenny Mwaisabula.
    Mwaisabula akaendelea na kazi hadi msimu wa 2005, lakini baadaye mwaka huo akaondolewa na kurejeshwa Chamangwana., ambaye alifanya kazi hadi 2007 alipompsha Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’.
    Micho aliondoka kwa sababu ambazo hadi leo bado hazieleweki, kwani alikubalika na timu ilikuwa inafanya vizuri. Alipoondoka Micho, timu akabakia nayo, aliyekuwa kocha wa makipa, Mkenya Razack Ssiwa.
    Ssiwa akaiongoza Yanga kutwaa Kombe la Tusker mwaka 2007 mjini Mwanza, lakini aliporudi kwenye ligi, timu inafanya vibaya, naya akatupiwa virago na kurejeshwa Chamangwana.   
    Chamangwana naye akaondolewa na kuajiriwa tena Mserbia, Profesa Dusan Savo Kondic, aliyekuja na Wasaidizi wawili, Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan. Kondic naye mwaka 2010 akafukuzwa na kuajiriwa Mserbia mwenzake, Kostadin Papic, ambaye naye alifukuzwa na kuajiriwa Mganda Sam Timbe.
    Timbe pamoja na kuipa timu Kombe la nne la Kagame mwaka jana, alifukuzwa miezi miwili baadaye na kurejeshwa Papic, ambaye pia hata kabla msimu uliopita wa Ligi Kuu haujamalizika, akatupiwa virago na kuajirwa Mbelgiji, Saintfiet.
    Saintfiet amehitimisha historia yake Yanga ndani ya siku 80, akicheza mechi 14, akishinda 12, sare moja na kufungwa  mbili- huku akiacha Kombe la tano la Kagame Yanga. Kwaheri Mtakatifu Tom, hiyo ndiyo Yanga!


    MAKOCHA YANGA TANGU 1991
    1.          1991: Syllersaid Mziray(marehemu)
    2.          1993: Nzoyisaba Tauzany (marehemu) (Burundi)
    3.          1995: Tambwe Leya (marehemu) (DRC)
    4.          1997: Sunday Kayuni
    5.          1997: Steve McLennan (Uinegereza)
    6.          1998: Tito Mwaluvanda(marehemu)
    7.          1999: Raoul Shungu (DRC)
    8.          2001: Charles Boniface Mkwasa
    9.          2002: Jack Chamangwana (Malawi)
    10.        2004: Jean Polycarpe Bonganya (DRC)
    11.        2004: Syllersaid Mziray (marehemu)
    12.        2005: Kenny Mwaisabula
    13.        2006: Jack Chamangwana (Malawi)
    14.        2007: Milutin Sredojevic ‘Micho’ (Serbia)
    15.        2007: Razack Ssiwa (Kenya)
    16.        2007: Jack Chamangwana (Malawi)
    17.        2008: Dusan Kondic (Serbia)
    18.        2010: Kostadin Papic (Serbia)
    19.        2011: Sam Timbe (Uganda)
    20.        2011: Kostadin Papic (Serbia)
    21.        2012: Tom Saintfiet    (Ubelgiji)

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWAHERI MTAKATIFU TOM, HIYO NDIYO YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top