• HABARI MPYA

    Monday, September 24, 2012

    TFF YAFAFANUA KANUNI, YANGA KUTOPOKONYWA POINTI ZA JKT

    Wachezaji wa Yanga wakishangilia 4-1 za JKT

    Na Mahmoud Zubeiry
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa ufafanuzi kuhusu kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, juu ya matumizi ya wachezaji wa kigeni na kusema kwamba Yanga ilikuwa sahihi kutumia wachezaji wake wote watano katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu, waliyoshinda mabao 4-1 juzi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ofisa wa Habari wa TFF, Boniphace Wambura ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba kanuni za sasa za Ligi Kuu, zinairuhusu klabu kutumia wachezaji wote watano wa kigeni waliodhinishwa kucheza ligi.  
    Mapema leo kulikuwa kuna hofu kwa Yanga kupokonywa pointi tatu ilizovuna kutokana na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na kuzidisha idadi ya wachezaji wa kigeni.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Wallace Karia ni kama hajui vema kanuni, baada ya kuiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni, lakini itaruhusiwa kutumia watatu tu kwa wakati mmoja.
    Alisema mabadiliko ya kanuni za wachezaji wa kigeni, kutoka watano hadi 10 kusajiliwa na watano kucheza kwa wakati mmoja, yataanza kutumika msimu ujao.
    “Tunatarajia kukutana keshokutwa kupitia ripoti za mechi zote, ikiwemo mechi ambayo Emmanuel Okwi alimpiga mchezaji mwenzake ngumi, baada ya kikao tutatoa ripoti ya maamuzi,”alisema Karia.
    Jumamosi, Yanga ikimenyana na JKT Ruvu, Mgahan Yawe Berko, alianza langoni, Wanyarwanda Mbuyu Twite alicheza beki ya kulia, Haruna Niyonzima alicheza kiungo cha juu, Mrundi Didier Kavumbangu na Mganda Hamisi Kiiza walicheza mbele.  
    Kikosi cha Yanga siku hiyo kilikuwa; Yaw Berko, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan/Shamte Ally, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu/Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Simon Msuva.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAFAFANUA KANUNI, YANGA KUTOPOKONYWA POINTI ZA JKT Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top