• HABARI MPYA

  Thursday, September 27, 2012

  YANGA WAINGIA KAMBINI CHANGANYIKENI LEO, BAGAMOYO WAMEKUSHITUKIA

  Baadhi ya  wachezaji wa Yanga

  Na Mahmoud Zubeiry
  YANGA ya Dar es Salaam, inatarajiwa kuingia kambini leo katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu.
  Awali, Yanga ilipanga kwenda kuweka kambi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani jana, lakini maamuzi yamebadilika.
  Wakati Yanga, wanaingia kambini leo Changanyikeni, wapinzani wao wa jadi, Simba SC, tayari wapo visiwani Zainzbar tangu juzi saa 11:00 jioni wakijiandaa na mchezo huo wa kukata na shoka, ambao utarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport, kuanzia saa 1:00 usiku.
  Habari kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba timu hiyo itaingia kambini na itarejea mjini Jumapili kucheza na African Lyon, na baada ya mechi itarejea huko kuendelea kujiandaa na pambano la watani.
  Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua, kwa sababu mara ya mwisho timu hizo zilipokutana, Yanga ilifungwa mabao 5-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kipigo hicho ilidaiwa kilitokana na uongozi dhaifu chini ya Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na pia ilikuwa sababu ya kumuondoa madarakani kiongozi huyo na kufanyika uchaguzi mdogo, uliomuweka madarakani Yussuf Manji, Mwenyekiti mpya.
  Tangu wakati wa kampeni, miongoni mwa mambo ambayo wana Yanga wamekuwa wakiomba kutoka kwa Manji ni kulipiwa kisasi cha 5-0, ingawa kwa hali ya sasa ya timu hizo, ubora wao haupishani sana, hakuna hakika kama hilo litawezekana.
  Wakati huo huo, Yanga inaendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya huku habari zikisema, ipo kwenye mazungumzo na makocha watatu, wawili kutoka Brazil akiwemo kocha wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo na mwingine jina lake halikuweza kupatikana- pamoja na Raoul Shungu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili mmoja wao aje kufundisha timu hiyo.
  Habari kutoka ndani ya Yanga zimesema kwamba, mazungumzo na Maximo yanaendelea ingawa bado kuna ugumu, lakini wakati huo klabu hiyo inazungumza na kocha mwingine Mbrazil.
  Pamoja na Wabrazil hao, Yanga majuzi ilianza mawasiliano na kocha wake wa zamani, Shungu, arejee kufundisha timu hiyo.
  Mkakati wa Yanga ni kocha mpya awasili nchini kabla ya Oktoba 3, watakapomenyana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC na kulingana na hali halisi, Shungu ni mwalimu anayepewa nafasi zaidi kuja kufanya kazi tena Jangwani.
  Katika kipindi cha miaka mitatu ya kufanya kazi kwake Yanga, kutoka 1998 hadi 2000, Shungu aliipa Yanga Kombe la Afrika Mashariki na Kati, mwaka 1999 katika fainali zilizofanyika Kampala, Uganda na mataji kadhaa ya nyumbani, likiwemo Kombe la FA, Nyerere, Muungano na ubingwa wa Bara.
  Aliondoka Yanga baada ya kutofautiana na Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Tarimba Abbas baada ya kusema amekwenda Ufaransa kusoma kozi fupi ya FIFA, lakini aliporudi akaambiwa aonyeshe pasipoti yake kama viza ya nchini humo, akawa anapiga chenga, hivyo akaonekana muongo.
  Kilichofuatia, aliyekuwa kocha wa African Sports ya Tanga wakati huo, Charles Boniface Mkwasa akaajiriwa kama Meneja wa timu na baada ya muda mfupi, Shungu akaondolewa na kiungo huyo wa zamani wa Yanga, akapewa Ukocha Mkuu.
  Maximo ni kocha ambaye, wana Yanga wanampenda sana na ilikuwa aje kufundisha timu hiyo badala ya Mbelgiji aliyetupiwa virago, Tom Saintfiet lakini inadaiwa ‘alilishiwa sumu na wazandiki’, ila kwa sasa wana Jangwani wanajaribu tena bahati yao.
  Yanga ipo katika mchakato wa kusaka kocha mpya, baada ya kumtimua Saintfiet aliyedumu kwa siku 80 tu, ambaye sasa nafasi yake anakaimu Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro hadi hapo atakapopatikana kocha  mwingine.
  Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema matokeo mabaya na kutotii matakwa ya uongozi, ndio vimemfanya Saintfiet asitishiwe mkataba. Aidha, Sanga alikanusha madai kwamba eti kocha huyo amefukuzwa baada ya kutofautiana na Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji.
  “Timu ilipokwenda Mbeya, ikatoka sare na Prisons akalalamikia huduma, lakini sisi taarifa tulizozipata, yeye aliwaruhusu wachezaji kwenda kulewa disko baada ya mechi. Kuna mapungufu mengine mengi, ambayo hatuwezi kusema hadharani.
  Kwa mfano timu ilipotoka Mbeya, tulitaka iende moja kwa moja Morogoro, yeye akalazimisha timu irudi Dar es Salaam, tena iende tena Morogoro. Wachezaji wakachoka sana na hii tunaamini ilichangia hata kufungwa na Mtibwa.
  Timu iliporudi kutoka Morogoro, tukaamua iingie kambini, yeye akapinga akisema timu kubwa kama Barcelona Ulaya, hazikai kambini, yaani anataka atupangie kazi sisi, tukaona huyu mtu haendani na maadili ya uongozi na hatufai, tukaamua kusitisha mkataba wake,” alisema Sanga.  
  Saintfiet ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu ndani ya siku 80 tangu ajiunge nayo Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi hizo amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
  Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAINGIA KAMBINI CHANGANYIKENI LEO, BAGAMOYO WAMEKUSHITUKIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top