• HABARI MPYA

  Tuesday, September 25, 2012

  SIMBA SC WAENDA ZANZIBAR ASUBUHI HII

  Simba SC

  Na Mahmoud Zubeiry
  SIMBA SC inaondoka leo asubuhi kwenda Zanzibar kuweka kambi ya kujiandaa na pambano la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
  Habari kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba timu hiyo itaondoka na boti ya saa 3:00 kwenda kisiwani humo kwa maandalizi ya kuendeleza ‘mila’ ya kuwanyanyasa wapinzani wao jadi, Yanga.
  Wekundu hao wa Msimbazi wanakwenda Zanzibar na Jumamosi watarejea mara moja Dar es Salaam kucheza na Prisons na baada ya hapo, watapanda bosi kurejea visiwani humo kuendelea na maandalizi yao.
  Katika mchezo huo, Simba SC, iko hatarini kumkosa mshambuliaji wake hodari wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, iwapo Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, itaamua kufuata kanuni za Ligi zinavyosema.
  Okwi alipewa kadi nyekundu ya moja kwa moja, kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT Ruvu, akilipa kisasi cha kuzewa rafu Jumatano iliyopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kwa mujibu wa kanuni hilo ni kosa la kufungiwa mechi tatu.
  Hata hivyo, Okwi anaweza kuokoka, iwapo tu ripoti za refa na Kamisaa zitambeba, ingawa hilo ni gumu, kwa sababu hakupewa kadi ya moja kwa moja kwa kucheza rafu wala kuushika mpira kwa makusudi, bali kupiga na hilo adhabu yake ni kukaa jukwaani mechi tatu.
  Tayari Okwi amekosa mechi moja ya juzi dhidi ya Ruvu Shooting na wakati, Kamati ya Ligi Kuu inakutana kesho, inatarajiwa kumuongezea mechi mbili zaidi, dhidi ya Prisons na dhidi ya Yanga na baada ya hapo atakuwa huru kuendelea kumtukia mwajiri wake.
  Siyo siri, kuelekea pambano la watani wa jadi, Okwi ni homa kwa Yanga, hasa wakikumbuka namna alivyowanyanyasa katika mechi iliyopita, akifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 5-0 na kusababisha mawili.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAENDA ZANZIBAR ASUBUHI HII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top