• HABARI MPYA

  Wednesday, September 26, 2012

  VODACOM WAKATAA KAMPUNI NYINGINE YA SIMU LIGI KUU, ZANTEL WAMELIWA NA LYON


  Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan akimkabidhi jezi, Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo kwa niaba ya klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam, katika hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro), Dar es Salaam wakati wa kutangaza kuingia mkataba wa kudhamini klabu hiyo kwa miaka mitatu. Wanaomfuatia Thadeo ni Meneja Mkuu wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ na Charles Otieno, Mkurugenzi wa Ufundi wa African Lyon. Kulia kabisa ni mchezaji chipukizi wa Lyon, Jarufu Magesa, ambaye anapelekwa na klabu Marekani kusoma na Kocha Muargentina wa African Lyon, Pablo Ignacio Velez.
  Dar es salaam 25th September 25, 2012, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesema suala la kuwepo kwa kipengele cha UpekeeEXCLUSIVITY” katika mkataba wa udhamini wa ligi kuu soka Tanzania bara kati ya kampuni hiyo na shirikisho la soka nchini - TFF ni la muhimu katika kuepuka migongano ya kimasilahi ya kibiashara miongoni mwa wadhamini.
  Mkuu wa Udhamini na Mawasiliano wa kampuni ya Vodacom Tanzania Bw Kelvin Twissa amesema kampuni ya Vodacom inajali na kuthamini maendeleo ya vilabu nchini na kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa kutoa fursa zaidi zinazolenga kukuza kiwango cha uwekezaji katika soka kwa masilahi ya vilabu na  taifa kwa ujumla.
  Twissa amesema katika kutambua umuhimu wa kupanua wigo wa uwekezazi katika ligi kuu ya Vodacom na maendeleo ya vilabu kwa ujumla, kampuni ya Vodacom Tanzania ilikubali kwa moyo mkunjufu kuruhusu vilabu kutafuta wadhamini wengine ambao siyo makampuni yanayofanya baishara sawa na Vodacom.
  Twissa alikuwa akizungumza katika kikao cha pamoja kilichowakutanisha Shirikisho la Soka Tanzania – TFF, Kamati ya Ligi Kuu na Mdhamini Mkuu kampuni ya Vodacom Tanzania  kilichoketi jana jijini Dar es salaam.
  “Tunatambua na kuheshimu utayari wa makampuni mengine ambayo yapo tayari kushirikiana na sisi katika kudhamini Ligi kuu ya Vodacom nasi tupo tayari kushirikiana nao na hivyo kuleta  maendeleo ya mpira wa miguu nchini”Alisema Twissa
  “Vodacom Tanzania inajivunia kuwa wadhamini wakuu wa ligi hii,tumeamua kuboresha udhamini wetu kwa sababu tunatambua umuhimu wa michezo kwa Taifa letu, sasa michezo si kwa ajili ya burudani tu bali imekuwa chanzo cha ajira na kuboresha maisha ya wanaojihusisha nayo,” Aliongeza Twissa.
  “Tunaviomba vilabu  vinavyoshiriki ligi kuu, vyombo vya habari na umma kwa ujumla kutambua kuwa azma ya Vodacom ni kuona mpira wa miguu unasonga mbele zaidi na ndio maana tumekuwa katika udhamni huu kwa zaidi ya miaka saba tukipitia vipindi tofauti lakini hatukuwahi kukata tamaa. Hivyo si vyema wakati huu soka yetu inapokua tukaruhusu hali inayoweza kusababisha changamoto katika uwekezaji wa soka.” Aliongeza Twisa
  Twissa amesema kampuni ya Vodacom itaendelea kushirikiana na TFF, Kamati ya Ligi na wadau wengine wote wa mpira wa miguu nchini katika kukuza uwekezaji kwa kusaidia vilabu kupata wadhamini watakaosaidia maendeleo ya vilabu hivyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VODACOM WAKATAA KAMPUNI NYINGINE YA SIMU LIGI KUU, ZANTEL WAMELIWA NA LYON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top