• HABARI MPYA

  Sunday, September 30, 2012

  YANGA KAZINI LEO LIGI KUU LEO

  11 wa kuaminika Yanga

  Na Mahmoud Zubeiry
  YANGA SC inashuka dimbani leo, kumenyana na African Lyon katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huo ukiwa mchezo wa mwisho kabla ya kumenyana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC Jumatano.
  Mechi hiyo itaanza saa 11:00 jioni na kurushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini.
  Yanga leo, itakuwa na kocha mpya kwenye benchi Mholanzi, Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, aliyewasili juzi na kusaini mkataba wa mwaka jana.
  Brandts amesema kwamba atajitahidi kadiri ya uwezo wake, kuhakikisha anaiongoza timu hiyo kushinda mechi ya leo na Jumatano dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC ingawa anajua utakuwa mtihani mgumu.
  Brandts alisema hayo, baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo mbele ya Waandishi wa Habari, katika Mkutano uliofanyika makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam asubuhi hii.
  Alisema kwanza anaushukuru uongozi wa klabu hiyo kuwa kumuamini, na anaafiki kwa kiasi kikubwa kupewa nafasi ya kurithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet, aliyetupiwa virago wiki iliyopita, baada ya kuitumikia Yanga kwa siku 80.
  “Muhimu kwangu, nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kuipa matokeo mazuri klabu kwa asilimia mia moja. Nilikuwa Uholanzi, nikapigiwa simu na Mwenyekiti, Yussuf Manji, akaniambia anataka nije kufanya kazi Yanga, nilikuwa nina ofa nyingi, ila nilivutiwa naye (Manji), aliponiambia falsafa na sera za klabu, anataka kuindeleza klabu.
  Kitu kingine ni kuhusu timu, kama kocha, kweli tuntaka kushinda kila mechi, lakini tunataka kucheza soka ya kuvutia. Jambo muhimu kwangu ni kufanya kila mchezaji mmoja mmoja acheze vizuri, na timu icheze vizuri, kwa sababu hakuna bora zaidi ya timu,”alisema.
  Brandts pia alizungumzia nihdamu, akisema; “Kuzingatia nidhamu, ni muhimu si hapa tu Afrika, hata Asia na Ulaya kwa sababu, ukitaka kuamka saa moja kamili amka saa moja kamili na ukitaka kujenga timu nzuri, muhimu kujituma, hata mimi nilipokuwa nacheza ilikuwa hivyo pia, ni muhimu kujivunia timu unayochezea na kila mchezaji anatakiwa kujivunia kuchezea Yanga,”alisema.
  Kuhusu kazi, alisema; “Kitu kingine, kuna mechi kesho na kuna mechi Jumatano, dhidi ya Simba itakuwa ngumu sana, tutafanya kila tunachoweza kuhakikisha tunashinda, naijua Yanga nimekuja hapa miaka miwili, ni timu nzuri. Sasa nakwenda kujaribu kuboresha timu, najiona mwenye bahati kusaini mkataba na timu hii,”alisema.
  Brandts alikuja mwaka jana na mwaka huu kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, akiwa na APR ya Rwanda na mara zote, Yanga iliibuka bingwa, mwaka jana ikifundishwa na Mganda Sam Timbe na mwaka huu ikifundishwa na Mbelgiji, Saintfiet.
  Mwaka jana, APR ilitolewa mapema katika kundi lake Morogoro, lakini mwaka huu ilifika hadi Nusu Fainali na kutolewa na Yanga. 
  Awali ya hapo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba wamepata kocha mzoefu wa soka ya Afrika ambaye amefanya kazi APR ya Rwanda.
  “Tulikuwa na makocha wengi katika mchakato, tumekuwa makini kutokana na matatizo yaliyojitokeza awali, tumekuwa makini na aina ya mikataba tunayoingia na makocha, ili tusije tukarudia makosa, tumezungumza naye matatizo yaliyotokea na kocha aliyemtangulia, ameridhika, ameona tuko sahihi, naye amesema yuko tayari kutimiza masharti ya mwajiri wake mpya,”alisema Sanga.
  Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi, aliwasili juzi majira ya saa 3:45 usiku katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na ndege ya KLM na kupokewa na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako na viongozi wengine, Abdallah Ahmad Bin Kleb, Seif Ahmad ‘Magari’ na Majjid Suleiman.
  Yanga, imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet, kutokana na kuwasili kwa Brandts, ambaye anaanza kazi mara moja leo.
  Kikosi cha Yanga kipo kambini, hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam na kabla ya kucheza na Simba Jumatano, kesho kitacheza na African Lyon, Uwanja wa Taifa pia.
  Mholanzi huyo aliyemaliza mkataba wake APR ya Rwanda baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga, baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
  Mtaalamu huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
  Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
  Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
  Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
  Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
  Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi miwili iliyopita na sasa amepata maisha mapya Yanga.
  Akiwa APR, Brandts alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
  Brandts atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia katika msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.
  Tayari Yanga imecheza mechi tatu za Ligi Kuu, kushinda moja, sare moja na kufungwa moja- hivyo inaachwa kwa mbali na wapinzani wake wakuu katika mbio za taji, Simba SC yenye pointi 12 na Azam FC yenye pointi 10, baada ya mechi nne.
  Ushindi leo ni muhimu kwa Yanga, kwani utaifanya iwasogelee wapinzani wake Azam kwa tofauti ya pointi mbili, kutoka nne hadi saba.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KAZINI LEO LIGI KUU LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top